29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Kiwanda cha Alizeti Hanan’g kuwainua wakulima kiuchumi

Na Mwandishi Wetu, Hanan’g

KUJENGEWA kiwanda cha kuchakata alizeti kwa jukwaa la wakulima wadogo na wasimamizi wa masoko ya alizeti Hanan’g (JUWAMA), kunatajwa kuwainua kiuchumi wakulima hao na kujiinua kiuchumi.

Akizungumza jana  na waandishi wa habari waliotembelea kiwanda cha jukwaa hilo kilichopo kijiji cha Galangala,wilayani hapa,Katibu wa jukwaa hilo,Andrew Jacob,alisema awali walikuwa wakiuza malighafi bila kuichakata ambayo ilikuwa haiwapi faida kubwa na walikuwa wakitumia madalali.

Alisema kwa kupitia madalali walikuwa wakipata hasara kwani wao ndiyo walikuwa wakionana na wateja hivyo wao kujikuta wakiuza malighafi kwa bei ndogo ila tangu wajengewe kiwanda hicho wamekuwa wakiuza mafuta na mashudu hivyo kupata faida tofauti na kipindi cha nyuma.

Alisema wadau waliowasaidia kujenga kiwanda hicho ambao ni Shirika lisilo la Kiserikali la Oxfam  Hongkong wakishirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la Ujamaa Community Resource Team (UCRT),kupitia mradi wa kuwainua kiuchumi wanawake na vijana wilayani humo.

Alisema mbali na kujengewa kiwanda hicho poa wamepewa zana mbalimbali kwa ajili ya kutumia kiwandani hapo ikiwemo mashine za kupepeta,kukamua na kuchuja mafuta,kiwanda kilichoanza kuchakata alizeti Julai mwaka jana.

“Baada ya kuona tunauza malighafi kupitia madalali,tuliamua kuzungumza na wadau wetu ambao ni Oxfam na UCRT,ili tuweze kuchakata wenyewe na hadi sasa tunaona tofauti kubwa,”alisema.

Katibu huyo alisema jukwaa hilo lenye wajumbe 174 linaundwa na vikundi sita ambapo kwa pamoja kupitia kiwanda hicho wameweza kuongeza mnyororo mzima wa thamani ya zao hilo.

Alisema kuanzia mwaka jana hadi Agosti mwaka huu wamechakata magunia 721 ya wanajukwaa hilo,ambapo kati ya gunia hizo gunia 636 zililipiwa na kupata Sh milioni 3.81 ambapo mbali na kuchakata mazao ya kikundi hicho pia wanachakata alizeti kutoka kwa wakulima wengine.

Alisema mbali na kuchakata mazao ya wanakikundi wamekuwa wakichakata mazao ya wananchi wengine ambapo hadi sasa jukwaa hilo limekusanya Sh 23.4 milioni ambazo zimegawanywa kwenye vikundi na nyingine zikiwa kwenye akaunti kuu ya jukwaa hilo.

Naye Martha Sule,alishukuru kwa elimu ya ujasiriamali kwani imewasaidia kwa kiwango kikubwa kwani awali katika jamii hiyo ya kifugaji wanawake hawakuwa wanajitegemea hivyo kujikuta wanategemea waume zao.

Alisema baada ya elimu hiyo akina mama wameanza kujitegemea na kukopa kupitia vikundi vyao na faida wanayopata kuitumia kwa ajili ya miradi mingine.

Alisema awali maisha ya wanawake kiuchumi yalikuwa magumu kwani walikuwa wanategemea waume zao ila kwa sasa kupitia jukwaa hilo wameanzisha vikundi vya kuweka na kukopa ambavyo vinawasaidia kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

“Tunawashukuru wadau wetu kwani kwa sasa hivi kuna tofauti kubwa ya mama aliyepo kwenye jukwaa na ambaye hayupo,sasa hivi naweza kununulia watoto nguo za shule na mahitaji mengine ya nyumbani na nimeweza kubadilisha maisha yangu na familia kwa ujumla,” amesema.

Kwa upande wake, Mratibu Msaidizi wa program hiyo kutoka UCRT,Albert Masaju,alisema kwa kushirikiana na Oxfam waliamua kujiwekeza kwenye kutoa elimu kwa jamii ya kifugaji ambapo wameanzisha mabaraza ya wanawake ya haki na uongozi.

“Hadi sasa tuna mabaraza matano na lengo la kuyaanzisha ni kuhakikisha jamii inaweza kulinda,kutetea na kujali haki za wanawake ili baadaye tuwe na jamii inayoheshimu haki sawa kwa wanawake,”alisema.

Akizungumzia mradi wa kilimo cha umwagiliaji,alisema kupitia eneo lenye ukubwa wa hekari 13 walilopewa na serikali ya kijiji kama sehemu ya shamba darasa linalotumiwa na wanakikundi hao,hekari tatu zitatumika kwa ajili ya kilimo hicho cha matone.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles