Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
MZUNGUKO wa saba wa Ligi Kuu Tanzania Bara, unatarajiwa kuendelea leo kwa viwanja tofauti nchini, ambapo Wekundu wa Msimbazi, Simba, wanatarajia kuwavaa Njombe Mji katika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.
Simba watakutana na Njombe Mji wakiwa na kumbukumbu ya kutoka suluhu dhidi ya Mtibwa Sugar, kwenye mchezo uliopigwa katika dimba hilo.
Hadi sasa Wekundu hao wa Msimbazi wanashika usukani kwenye msimamo wa ligi, huku wakijikusanyia pointi 12, wakiwa sawa na Yanga, Mtibwa pamoja na Azam FC, wakitofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Wanamsimbazi hao watakuwa wakihitaji ushindi ili waendelee kuongoza ligi kutokana na kufungana pointi kwa takribani timu tatu.
Kikosi hicho kitawavaa Njombe Mji wakiendelea kuwakosa nyota wao, John Bocco na Salim Mbonde ambao ni majeruhi, huku wakiwa na kocha mpya msaidizi, Masud Djuma, aliyetua nchini juzi kurithi mikoba ya Jackson Mayanja aliyebwaga manyanga kwa sababu ya matatizo ya kifamilia.
Upande wao Njombe Mji ambao wamepanda ligi msimu huu wakiwa pamoja na Lipuli FC na Singida United, wataingia uwanjani wakiwa wanahitaji ushindi ili kujiweka kwenye mazingira mazuri kwenye msimamo wa ligi kutokana na kuanza kwa kuvurunda kwenye mechi za awali.
Wakati matajiri wa jiji, Azam FC, ambao wapo ugenini watakutana na Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, wakihitaji ushindi kutokana na wapinzani wao kuwa na historia nzuri wakiwa nyumbani.
Azam mchezo uliopita walitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mwadui FC, mchezo uliopigwa Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga, ambao kwa sasa wanashika nafasi ya nne huku wakijikusanyia pointi 12 wakiwa sawa na Simba, Yanga na Mtibwa Sugar wakitofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Akizungumzia mchezo huo kocha mkuu, Joseph Omog, alisema anawaheshimu Njombe Mji, kwani ni timu nzuri hivyo lazima wawe makini kuhakikisha wanapata pointi tatu muhimu.
“Baada ya kutoka sare kwenye mchezo uliopita niliyafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza ili yasijirudie, hivyo tunaamini ushindi utakuwa kwetu,” alisema.
Upande wake kocha msaidizi wa Njombe Mji, Mrage Kabange, alisema anaifahamu Simba ni timu kubwa na ina wachezaji wazuri lakini haiwezi kuwa sababu ya wao kufungwa kirahisi.
“Licha ya Simba kuwa na kikosi imara, lakini wote tunashiriki ligi kuu, hivyo tutapambana na kuwa makini ili tuweze kupata ushindi ugenini,” alisema.
Michezo mingine itakuwa ni kati ya Singida United, ambao watakaribishwa na Ndanda FC kwenye dimba la Nangwanda Sijaona Mtwara, wakati Mbeya City watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Huku Wakata miwa, Mtibwa Sugar wakiwakaribisha Tanzania Prisons kwenye dimba la Manungu, Morogoro na Lipuli FC wakikutana na Majimaji, Samora mjini Iringa.