MOHAMED KASSARA -DAR ES SALAAM
BAADA ya kulazimishwa suluhu na Mwadui FC katika mchezo wao uliopita, Kocha Mkuu wa Namungo, Hitimana Thiery amesema kikosi chake kitamaliza hasira zao leo kwa kuhakikisha kinaichapa KMC katika mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Namungo ambayo imejikusanyia pointi saba ilizovuna baada ya kushuka dimbani mara tatu , itakuwa ugenini kuikabili KMC inayoburuza mkia katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa haina pointi hata moja.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Thiery alisema licha ya kwamba watakuwa ugenini benchi la ufundi na wachezaji wao wamekubaliana kukamilisha dakika 90 wakiwa na matokeo ya ushindi.
“Matokeo hayakuwa mazuri kwetu japo hatujapoteza lakini tumesahau.
“Sasa akili zetu zipo katika kupata pointi tatu kwa KMC, tunafahamu ugumu ulioko lakini kwa namna tulivyojipanga sina shaka tutatimiza lengo.
“Kwenye soka unaweza kupata pointi popote kama utakuwa umejiandaa vizuri, tuna uzoefu wa kutuwezesha kutambua mazingira ya ugenini na nyumbani, tunafahamu tunatakiwa kucheza vipi ili tupate matokeo mazuri,”alisema mkufunzi huyo raia wa Burundi.
Ligi hiyo pia itaendelea kwenye viwanja vingine vitano Singida United itaikaribisha Mbao FC Uwanja wa Namfua mjini Singida, Alliance itakuwa ugenini Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga kuumana na Mwadui FC.
Wagosi wa Kaya, Coastal Union watakuwa wageni wa Ruvu Shooting, Uwanja wa Mabatini Pwani, wakati Mtibwa Sugar itakuwa nyumbani Uwanja wa Manungu katika Mkoa wa Morogoro kukabiliana na Tanzania Prisons, huku Biashara United ikipepetana na JKT Tanzania kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Karume, Musoma.