Na MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM    |  Â
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amemwandikia barua Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Dk. John Magufuli, akimwomba kujiuzulu wadhifa wake huo.
Kinana ambaye amekuwa Katibu Mkuu wa CCM tangu mwaka 2012, taarifa ambazo gazeti hili limezipata kutoka katika vyanzo vyake na vile vilivyo karibu na mwanasiasa huyo, zinadai safari hii Rais Magufuli ameridhia ombi lake hilo baada ya kumkakatalia huko nyuma.
Julai 2016, katika Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM ambao Rais mstaafu Jakaya Kikwete alimkabidhi uenyekiti wa CCM Rais Magufuli, ikiwa ni miezi minane tangu aingie madarakani, Kinana aliwasilisha barua ya kujiuzulu nafasi hiyo, lakini kiongozi huyo wa nchi aliikataa akimwomba amsaidie kwa sababu ya uzoefu wake.
Rais Magufuli, pia aliwataka manaibu katibu wakuu wawili na sekretarieti nzima ya chama hicho, kuendelea na kazi.
Taarifa zinaeleza Kinana anatarajiwa kutangaza uamuzi wake wa kujiuzulu kesho wakati vikao vya juu vya chama hicho kwa maana ya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) vitakapoanza kuketi, Ikulu, Dar es Salaam.
Gazeti hili jana mara kadhaa lilimtafuta Kinana, lakini halikuweza kumpata.
Limedokezwa na vyanzo vyake vya uhakika kuwa uamuzi wa Kinana kuomba kuondoka katika nafasi hiyo, unatokana pamoja na sababu nyingine, kuona yapo mambo ambayo hashirikishwi.
Inaelezwa miongoni mwa mambo ambayo Kinana anaona hakushirikishwa kwa nafasi yake na amepata kusikika akisikitika kwa watu wake wa karibu, ni suala zima la uundwaji wa kamati kuchunguza mali za CCM.
Tayari ripoti ya kamati hiyo ilikabidhiwa kwa Rais Magufuli hivi karibuni na kimsingi huenda ikajadiliwa na wahusika kuchukuliwa hatua katika vikao hivyo vinavyoanza kuketi kesho.
Jambo jingine ni uteuzi wa wagombea ubunge katika majimbo ya Siha na Kinondoni, ambalo wana CCM wengi pia walilamika kuwa utaratibu wa chama hicho ulikiukwa.
Hata kabla ya Kinana hajaomba kujiuzulu, mjadala wa yeye kuondoka kwenye nafasi hiyo licha ya kudumu kwa muda mrefu na hata wakati fulani kutulia, ulirejea tena kwa kasi juzi na jana baada ya Rais Magufuli kuonekana akifanya vikao bila yeye kuwapo.
Pamoja na kwamba Ikulu haijaeleza chochote, lakini mikutano ambayo Rais Magufuli ameifanya kwa siku mbili mfululizo juzi na jana, yote akiwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula huku Kinana akiwa hayupo, tayari ilianza kujenga hisia kwamba huenda moja ya ajenda zao ilikuwa ni kujadili mtu ambaye atarithi nafasi ya Kinana.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, ilieleza Rais Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM-Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein pamoja na Mangula.
Pasipo kufafanua, taarifa hiyo ilieleza viongozi hao wamezungumzia masuala mbalimbali yanayohusu CCM na Serikali.
Juzi, Rais Magufuli alikutana na Rais mstaafu Benjamin Mkapa na Mangula, na kufanya mazungumzo ambayo ajenda yake haikuwekwa wazi.
Wakati zikiibuka taarifa za Kinana kuondoka sasa licha ya tetesi zake kudumu kwa muda mrefu kutokana na kutoonekana sana kwenye shughuli nyingi za CCM, tayari kulishazuka mjadala wa nani atakuwa Katibu Mkuu wa chama hicho kikongwe barani Afrika.
Katika mjadala huo, licha ya kwamba jina la Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba liliwahi kutajwa, lakini kitendo cha Rais Magufuli kukamilisha nafasi mbili za uteuzi wa wajumbe wa NEC kikatiba kwa kuwateua Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda na kada wa CCM, ambaye pia ni mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Makongoro Nyerere, kumeongeza namba ya watu wanaotajwa kumrithi Kinana.
Watu ambao wanafuatilia mwenendo wa kisiasa wa CCM, wanasema kwa Pinda inaweza kuleta shida kwa sababu ya kuwahi kwake kushika wadhifa mkubwa wa uwaziri mkuu.
Kwa sababu hiyo wanasema mtu ambaye anatajwa sana ni Makongoro ambaye CCM inaweza kumpa nafasi hiyo ili kuionyesha jamii kwamba inarudi kwenye misingi ya Baba wa Taifa.
Watu wengine waliowahi kushika nafasi ya Katibu Mkuu CCM wakati huo wakijulikana kama makatibu wakuu watendaji ni pamoja na Pius Msekwa (1977-1980) na Daudi Mwakawago (1980-1982).
Baada ya cheo hicho kubadilishwa na kuwa Katibu Mkuu, walioshika nafasi hiyo ni Rashid Kawawa (1982-1990), Horace Kolimba (1990-1994) Lawrence Gama (1994-1996), Philip Mangula (1996-2006), Yusuf Makamba (2006-2011) na Wilson Mkama (2011-2012).
Kinana anaondoka huku akiwa ameitumikia CCM kwa muda mrefu akipata kufanya kazi na marais wote wa Tanzania, kuanzia Mwalimu Nyerere hadi Rais Magufuli.
Ndani ya utumishi wake CCM, hususani nafasi ya ukatibu mkuu ambayo ameitumikia kwa takribani miaka saba, alifanya operesheni mbalimbali za kukijenga chama.
Miongoni mwa operesheni hizo ni ile ya kuzunguka nchi nzima kushiriki mambo mbalimbali ya kijamii ambayo iliibua madhaifu mbalimbali ya watendaji wa Serikali ya awamu ya nne kupitia wizara mbalimbali.
Ikumbukwe operesheni hiyo ndiyo iliibua mawaziri mizigo, ambao utendaji wao ulionekana kulalamikiwa na wananchi katika maeneo ambayo Kinana na timu yake walipita.
KINANA NI NANI?
Abdulrahman Kinana alizaliwa miaka 66 iliyopita jijini Arusha, na baada ya masomo ya awali ya shule ya msingi na sekondari, alikwenda kumalizia Chuo Kikuu cha Harvard huko Marekani.
Mkongwe huyo wa siasa nchini, aliyebobea kwenye mikakati, aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini kama Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa na Waziri wa Ulinzi.
Kabla ya kushika nyadhifa hizo, Kinana aliwahi kulitumikia Jeshi la Wananchi (JWTZ) kwa miaka 20 hadi alipostaafu mwaka 1972 akiwa na cheo cha Kanali.
Pia mwanasiasa huyo aliwahi kuwa Spika wa kwanza wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kuanzia mwaka 2001 hadi 2006.
Jemedari huyo wa siasa za CCM, amewahi kuongoza kampeni za urais ndani ya chama hicho tangu mwaka 1995 wakati wa Rais mstaafu Mkapa, akiingia madarakani na kipindi cha Rais mstaafu Kikwete akiwa kama meneja wa kampeni.
Kinana ambaye alikuwa mbunge wa Arusha Mjini kwa miaka 10, kabla ya hapo anaelezwa kuwa alikuwa mmoja wa vijana tegemeo wa chama cha TANU.
Nyadhifa nyingine ambazo Kinana amewahi kushika ni pamoja na Mjumbe wa Tume ya Maafa na Usaidizi, Mjumbe wa Msalaba Mwekendu na Mwezi Mchanga, Mwakilishi wa Rais, Nchi za Maziwa Makuu, Mwenyekiti wa Viwanda vya Pharmaceutical Industries na Diamond Shipping Company.
Pia aliwahi kuwa Mjumbe wa Bodi ya Tumbaku, Msuluhishi wa Amani wa Rwanda, Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Ulinzi na Usalama wa nchi za SADC na Mkuu wa Ujumbe wa Nchi zilizo mstari wa mbele SADC, OAU, UN.
Aliwahi pia kutumikia nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Stanbic Bank Tanzania tangu Septemba 5, 2007 na kuwa Mkurugenzi wa African Risk and Insurance Services Ltd.