ROSEAU, DOMINICA
KIMBUNGA Maria kilichopata nguvu na kufikia kiwango cha ngazi ya tano kimepiga kisiwa cha Caribbean cha Dominica kikiwa na mwendo kasi wa kasi ya kilomita 260 kwa saa.
Waziri Mkuu wa Dominica, Roosevelt Skerrit aliandika katika mtandao wa Facebook kuwa paa la nyumba yake limeng’olewa na nyumba yake kufurika maji.
Maria kinapitia njia ambayo kimbunga kama hicho cha Irma kilisababisha uharibifu mkubwa wakati kikipitia eneo hilo mwezi huu.
Kisiwa kilicho karibu cha Martinique kiliwekwa katika tahadhari huku kingine cha Ufaransa cha Guadeloupe kikiwaamrisha watu kuondoka.
Baaadhi ya sehemu hizo bado zinarejea hali ya kawaida baada ya kupigwa na kimbunga Irma , ambacho ni kimbunga cha kiwango cha tano kilichosababisha vifo vya watu 37 na kusababisha hasara ya mabiliono ya dola.
Watabiri wa hali ya hewa walionya kuwa mvua kubwa inayosababishwa na kimbunga hicho inaweza kusababisha mafuriko na maporomoko ya udongo ya kutishia maisha.