PYONGYANG, KOREA KASKAZINI
KIONGOZI wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, ameituhumu Marekani kwa kuwa na nia mbaya kwenye mazungumzo kuhusu mpango wa nyukilia unaofanywa na nchi yake.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Korea Kaskazini, Kim Jong Un alisema hayo wakati akiwa kwenye mazungumzo na Rais wa Urusi, Vladimir Putin.
Kim amedaiwa kumweleza Putin kuwa Marekani ilichukua msimamo wa upande mmoja kwa nia mbaya wakati wa mkutano wa kilele kati ya Kim na Rais wa Marekani, Donald Trump, miezi miwili iliyopita nchini Vietnam.
Kim amekaririwa akisema amani na usalama kwenye rasi ya Korea inategemea mtazamo wa Marekani katika siku zijazo na nchi yake itajiweka tayari kwa hali yoyote itakayojitokeza.
Mkutano kati ya Kim na Trump ulivunjika bila makubaliano baada ya Marekani kusema Korea Kaskazini ilitaka kuondolewa vikwazo vya uchumi haraka bila ya kueleza itafanya nini kuhusu mpango wake wa nyuklia.
Putin alitoa wito wa kulegezwa kwa vikwazo vilivyopo akisema Urusi pia inaunga mkono juhudi za kutuliza mzozo kwenye Rasi ya Korea.