RAIS Jakaya Kikwete amefanya uteuzi wa wakuu wapya wanne wa mikoa, huku akiwahamisha sita na wengine watatu kuwapangia kazi nyingine.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na kusainiwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, wakuu wapya wa mikoa walioteuliwa ni Halima Dendego anayekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dk. Ibrahim Msengi, Katavi, Amina Masenza, Iringa na John Mongella, Kagera.
Taarifa hiyo ilisema kabla ya uteuzi huo, Halima Dendego alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dk. Msengi, Moshi, Masenza, Ilemela na Mongella Arusha Mjini.
“Wakuu hao wapya wa mikoa watahapishwa leo saa saba mchana, Ikulu, Dar es Salaam,” inasema taarifa hiyo.
Kazi mpya
Taarifa hiyo inasema kuwa, wakuu wa mikoa ambao watapangiwa kazi nyingine ni Kanali Mstaafu Fabian Massawe aliyekuwa Kagera, Dk. Christine Ishengoma, Iringa na Kanali Joseph Simbakalia, Mtwara.
Vituo vipya
Wakuu wa Mikoa ambao wamehamishwa vituo vya kazi ni Magesa Mulongo kutoka Arusha kwenda Mwanza, Dk. Rehema Nchimbi Dodoma kwenda Njombe, Ludovick Mwananzila Lindi kwenda kwenda Tabora, Kepteni Mstaafu Anseri Msangi kutoka Njombe kwenda Mara na Everist Ndikilo Mwanza kwenda kwenda Arusha.
Wengine waliohamishwa ni Luteni Mstaafu Chiku Galawa kutoka Tanga kwenda Dodoma, Dk. Rajab Rutengwe Katavi kwenda Tanga, Fatma Mwasa, Tabora kwenda Geita, na Magalula S. Magalula, Geita kwenda Lindi.
“Wakuu wa Mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Kilimanjaro, Manyara, Mbeya, Morogoro, Pwani, Rukwa, Shinyanga, Ruvuma, Singida na Simiyu watabakia kwenye vituo vyao vya sasa,” inaeleza taarifa hiyo.
Panga la makatibu wakuu
Rais Kikwete pia ameteua Makatibu Wakuu wapya wanne na kuhamisha mmoja.
Walioteuliwa ni Dk. Donan Mmbando atakayekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Yohana Budeba, Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mhandisi Mbogo Futakamba, Wizara ya Maji na Dk. Adelhelm Meru, Wizara ya Utalii na Maliasili.
Kabla ya uteuzi huo Dk. Mmbando alikuwa Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Budeba, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Uvuvi na Mifugo, Mhandisi Futakamba, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji na Dk. Meru, Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA).
Waliohamishwa ni Maimuna Tarishi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii kwenda Wizara ya Katiba na Sheria.
Kuhusu uteuzi na uhamisho wa Makatibu Tawala wa Mikoa, Rais Kikwete amemteua Charles Pallangyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Adoh Steven Mapunda, Mkurugenzi Mtendaji, Manispaa ya Bukoba kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Severine Kahitwa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro na Dk. Faisal Issa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza.
Wakati huo huo, Rais Kikwete amemteua Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia, ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, kuwa Mkurugenzi Mkuu wa EPZA.
Uteuzi huo ulianza jana ambapo makatibu wakuu hao pamoja na makatibu tawala nao wataapishwa leo Ikulu, Dar es Salaam.
Pamoja na hili Rais Kikwete amefanya uteuzi wa Wakuu wapya wa Wilaya, kuhamisha baadhi yao na kutengua uteuzi wa baadhi ambapo taarifa kamili itatolewa na Waziri Mkuu baada ya kuwa wamepangiwa vituo vya kazi