24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

KIGOGO TUME YA UCHAGUZI KENYA AJIUZULU

NAIROBI, KENYA


OFISA wa ngazi ya juu katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Kenya (IEBC), Dk. Roselyn Akombe, amejiuzulu siku nane kabla ya uchaguzi wa rais na kuikimbia nchi hiyo.

Katika taarifa aliyotoa akiwa New York, Marekani anakoishi na kufanya kazi Umoja wa Mataifa (UN), ofisa huyo amewalaumu wenzake kwa misimamo ya upendeleo wa kisiasa na kuwa uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Oktoba 26 hautaaminika.

Kujiuzulu kwa Dk. Akombe ambaye ni miongoni mwa makamishna saba wa IEBC, ni pigo la hivi karibuni kwa mchakato wa uchaguzi huo, katika nchi, ambayo imetumbukia katika mgogoro mbaya zaidi wa kisiasa kipindi cha muongo mmoja uliopita.

Akombe amesema katika hali ya sasa IEBC haiwezi kuandaa uchaguzi huru na haki Oktoba 26, na hivyo hataki kuwa miongoni mwa wanaoukejeli uadilifu unaohitajika chaguzini.

Akombe ameongeza kuwa amekuwa akivumilia kwa miezi kadhaa katika tume hiyo huku akijiuliza swali la wajibu wake hasa katika chombo hicho.

Katika mahojiano na Shirika la Habari la Uingereza (BBC), Akombe amesema alihofia maisha yake na hivyo hawezi kurudi katika nchi yake hivi karibuni.

Ameelezea kuwa baadhi ya maafisa wa IEBC katika siku za hivi karibuni wanaishi wakihofia usalama wao kutoka kwa wanasiasa na maeneo ambayo yamekumbwa na maandamano.

Lakini pia amewalaumu wenzake kwa kutaka kufanya uchaguzi hata wakati maisha ya maafisa wake na wapiga kura yamo hatarini.

Kwa mujibu wa Dk. Akombe, uchaguzi hauwezi kuwa huru na wa haki wakati ambapo maafisa wako katika shinikizo za kisiasa na wanapata maelezo kuhusu mageuzi ya teknolojia na mitambo ya kuwasilisha matokeo ya uchaguzi katika dakika za mwisho.

Dk. Akombe amesema taifa halijachelewa sana kulizuia kutumbukia kwenye mzozo.

Wanaohitajika ni watu wachache waadilifu wanaoweza kusimama imara na kusema hatuwezi kuendelea na uchaguzi kwa namna ulivyopangwa kwa sasa, anasema.

Akombe ambaye alichukua likizo kutoka katika kazi yake UN ili kuhudumu IEBC ameiambia BBC kuwa amekimbilia Marekani baada ya kupokea vitisho kutoka kwa watu asiowajua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles