NAIROBI, KENYA
OFISA Mtendaji Mkuu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya, IEBC, Ezra Chiloba, ameomba likizo ya wiki tatu zikiwa zimebaki siku chache kabla ya zoezi la uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 26 mwaka huu. Chiloba amechukua likizo hiyo huku akiwa anaandamwa na viongozi wa muungano wa upinzani nchini humo, NASA ambapo wanamtuhumu kushiriki njama za kumsaidia Rais Uhuru Kenyatta kupata ushindi katika uchaguzi wa Agosti 8, mwaka huu.
Mara baada ya Mahakama ya Juu zaidi nchini humo kufuta matokeo ya urais, aliyekuwa mgombea wa muungano wa upinzani, Raila Odinga, alisema Ezra Chiloba, hatakiwi kuwa mmoja wa watendaji wa Tume ya Uchaguzi kwa sababu alisimamia uchaguzi uliojaa dosari na ukiukwaji wa sheria za uchaguzi.
Chiloba amechukua uamuzi binafsi wa kwenda likizo bila kutoa ufafanuzi zaidi juu ya hatua hiyo. Amesema utaratibu wa uchaguzi mkuu utaendelea kama ulivyopangwa na utazingatia agizo la Mahakama ya Juu.
“Hii ni mara ya kwanza nachukua likizo tangu kuzaliwa mwanangu. Ametimiza miaka miwili na wiki mbili,” alisema Chiloba alipozungumza na Shirika la habari la Reuters.
Wapinzani nchini humo wamekuwa wakishinikiza kuondolewa kwenye nyadhifa zao, Ezra Chiloba na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Wafula Chebukati na kutoa masharti kuwa wataitisha maandamano yasiyo na kikomo kama wangeendelea na nyadhifa zao.