Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM
WATAHINIWA 385,938 wa kidato cha nne, leo wanatarajiwa kuanza kufanya mitihani ya Taifa ya kumaliza elimu ya sekondari.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), Dk. Charles Msonde, alisema kati ya watahiniwa hao, 323,513 ni wa shule na 62,425 ni wa kujitegemea.
Alisema mitihani huo utaanza leo hadi Novemba 17,2017.
Dk. Msonde alisema maandalizi ya mitihani yameshakamilika na mitihani yote tayari imeshafika kwenye vituo husika.
Alisema kamati za mitihani za mikoa na halmashauri zihakikishe utaratibu wa uendeshaji wa mitihani unafuatwa.
Dk. Msonde aliwataka wanafunzi kuacha vitendo vya udanganyifu wakati wa kufanya mitihani kwa sababu wanaweza kufaulu bila kudanganya.
“Mliyojifunza yanatosha, fanyeni mitihani kwa kufuata utaratibu uliowekwa,” alisema Dk. Msonde.
Alionya kuwa baraza analoliongoza halitasita kuwafutia mitihani wote watakaojihusisha na udanganyifu.