Na ABRAHAM GWANDU,ARUSHA
VIONGOZI wa Serikali wametakiwa kuwa waangalifu wakati wote wanapotoa kauli zenye mwelekeo wa kupotosha ukweli kuhusu taaluma ya uandishi wa habari na wanahabari kwa ujumla.
Kauli hiyo ilitolewa Arusha jana na Mhariri Mtendaji Mkuu (GME) wa Kampuni ya New Habari 2006 Limited, Absalom Kibanda, wakati wa hafla ya kutoa tuzo ya Daud Mwangosi kwenye Mkutano Mkuu wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari (UTPC).
Mwandishi wa Habari, Azori Gwanda alitangazwa mshindi wa tuzo hiyo kwa mwaka huu.
Jopo la majaji wane, Ndimara Tegambwage, Eda Sanga, Keneth Simbaya na Aiman Duwe walipitia vipengele tofauti kumpata mshindi.
Kibanda ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo aliwaasa waandishi wa habari kuendelea kutumia taaluma yao kupinga kauli za aina hiyo kutoka kwa baadhi ya viongozi ambao aliwaita ni wajinga.
“Viongozi wawe waangalifu wa kauli na matendo yao kwa sababu kauli za viongozi zimekuwa kichocheo nyuma ya utekaji, utesaji na hata mauaji kwa waandishi wa habari.
“Wanapotoa mifano ya mauaji ya kimbali ya Rwanda kuwa yalichochewa na vyombo vya habari, huu ni upotoshaji na ndiyo maana baadhi ya wajinga wachache huchukulia ndio ukweli.
“Tuendelee kupinga mitizamo hii ya viongozi wetu… walioripoti kesi za mauaji yale katika mahakama ya kimataifa wanajua ukweli kuhusu idadi ya wahusika mpaka viongozi wa dini walikuwa wengi kuliko waandishi,” alisema Kibanda.
Alimshauri Rais John Magufuli kuchukua hatua za haraka dhidi ya matukio yanayofanywa na vyombo vya dola ya kuwakamata, kuwapiga na kuwatesa waandishi wa habari wanapotekeleza majukumu yao.
“Rais wetu asiishie tu kupongeza na kuvishukuru vyombo vya habari vinapoisifia Serikali, tunamsihi achukue hatua dhidi ya wote wanaotekeleza matukio haya,” alisema.
Alisema baadhi ya viongozi wa siasa wanaangalia maslahi yao hususan kipindi cha uchaguzi bila kujali athari za kauli na matendo yao.
Kibanda alisema iwapo hatua hazitachukuliwa sasa matukio hayo yakaachwa yaendelee, yatajenga taswira na roho ya kisasi kwa vizazi vingi vijavyo.
Awali, akizungumzia uamuzi wa kumpatia tuzo hiyo Gwanda, Mwenyekiti wa jopo la majaji waliofanikisha kupatikana mshindi, Ndimara, alisema wanahabari wanatakiwa kufanya kazi zao bila woga, vitisho wala ahadi tamutamu kutoka kwa watawala.