Kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema itasikilizwa siku tatu mfululizo kuanzia Novemba 27 hadi 29, mwaka huu katika Mahakama ya Wilaya ya Arusha.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Devota Msoffe amesema uamuzi huo ni kutokana na kesi hiyo kuwa nje ya wakati.
“Tutasikiliza kesi hii siku tatu mfululizo kwani iko nje ya wakati na natoa wito kwa mashahidi wa jamhuri kuitwa na kuwapo wakati wote wa kesi kwani tunarajia kufunga ushahidi wao Novemba 29,” amesema Hakimu huyo.
Awali, akimsomea maelezo ya awali mshtakiwa huyo, Wakili wa Serikali Agness Hyera katika kesi hiyo namba 440 ya mwaka 2016, amedai kuwa Lema anakabiliwa na shitaka moja la uchochezi ambapo anadaiwa kutenda kosa hilo Oktoba 22, mwaja jana katika eneo la Kambi ya Fisi, Kata ya Ngarenaro akiwa anahutubia mkutano wa hadhara.
Miongoni mwa maneno anayodaiwa Lema kutoa ni kuwa “Rais Magufuli akiendelea na tabia ya kudhalilisha demokrasia na uongozi wa upinzani iko siku taifa litaingia kwenye umwagaji wa damu,…. “Rais yeyote ambaye haheshimu mipaka ya sheria, mipaka ya Katiba, Rais huyo ataingiza taifa katika majanga na umwagaji damu, watu watajaa vifua, wakiamua kulipuka polisi hawa wala jeshi halitaweza kudhibiti uhalifu utakaojitokeza.”