Na UPENDO MOSHA-MOSHI
SHAHIDI wa tisa katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa Madini ya Tanzanite, Erasto Msuya, aliyeuawa kwa kupigwa risasi 22, amesema hakuona umuhimu wa kuchukua nguo za marehemu kama kielelezo cha ushahidi katika kesi hiyo.
Aliieleza mahakama kwamba hakuona umuhimu wa kuchora ramani katika eneo la pili la tukio ambalo ilikutwa pikipiki  namba T 316 CLP, aina ya Toyo ambayo ilitumika katika mauaji.
Shahidi huyo wa tisa ambaye pia ni Mkaguzi wa Polisi, Samuel Maimu, aliyasema hayo jana alipokuwa akitoa ushahidi katika Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi, alipokuwa akihojiwa na Wakili wa Utetezi, Emanueli Safari ambaye anamwakilisha mtuhumiwa wa tatu, Musa Mangu.
“Sikuwapo wakati marehemu anavuliwa nguo na pia sikuona umuhimu wa kukusanya nguo hizo kama kielelezo katika kesi hii.
“Pia, sijui baada ya kuvuliwa nani alikabidhiwa kwa sababu mimi siyo mpelelezi wa kesi mpaka ninayetakiwa kujua nguo ni sehemu ya ushahidi.
Mahojiano hayo yalikuwa kama ifutavyo.
Wakili: Shahidi hebu isaidie mahakama, ulisema wakati unaandaa ramani uliandaa ramani ya tukio lenyewe, ni wapi ulionyesha vielelezo?
Shahidi: Nilisema nilitoa katika mwili wa marehemu na sikuweka alama yoyote.
Wakili: Ulisema uliweka alama za kudumu katika eneo la tukio na kama mpelelezi ni lazima utajua masuala ya kijiografia, je unafahamu?
Shahidi: Ndiyo nafahamu
Wakili: Ulitumia vipimo gani katika ramani yako?
Shahidi: Futi ili kuonyesha mita
Wakili: Je ulianzia wapi?
Shahidi: Katikati ya lami
Wakili: Nani alikushikia futi wakati wa kupima?
Shahidi: Siwezi kukumbuka maana si sehemu ya ushahidi kwa sababu siyo kielelezo.
Wakili: Una elimu gani?
Shahidi: Elimu ya kidato cha sita.
Wakili: Tuambie katika kesi hii nani mpelelezi mkuu?
Shahidi: Kesi zote zipo kwa RCO na tunafanya kazi chini yake.
Wakili: Je, unaweza kukumbuka zilikuwa ni risasi ngapi ulizozikuta?
Shahidi: Ndiyo ni risasi 30 nilizitoa katika magazine.
Wakili: Kuna aina ngapi za risasi?
Shahidi: Nyingi
Wakili: Risasi hizo zilikuwa ni aina gani?
Shahidi: Ni za kawaida na zilikuwa hazina ncha kali.
Wakili: Je, wakati unafanya kazi hiyo, RCO alikuwa wapi?
Shahidi: Siwezi kujua.
Wakili: Ulisema katika eneo la tukio, kulikuwa na watu wengi ni wangapi?
Shahidi: Hapana siwezi kujua.
Wakili: Shahidi, katika ushahidi wako ulisema ulipigiwa simu na raia akikuarifu kuna pikipiki ilitelekezwa na washitakiwa na mlienda na timu yenu, mlikuwa wangapi?
Shahidi: Tulikuwa askari sita na ilikuwa ni timu kutoka katika ofisi ya RCO, Mkoa wa Kilimanjaro.
Wakili: Ulisema ulipima na futi, je, kutoka katika eneo alilokuwa marehemu hadi hapo ilipotelekezwa pikipiki, ilikuwa ni umbali gani?
Shahidi: Ilikuwa ni zaidi ya kilometa moja
Wakili: Je, eneo la pili ulichora ramani kama ulivyofanya katika eneo la kwanza?
Wakili: Hapana.
Wakili: Kwa nini?
Shahidi: Sikuchora kwa sababu ya uhalisia wenyewe wa eneo lenyewe. Ningefanya hivyo ningeweza kuidanganya mahakama kwa sababu eneo hilo lilikuwa limekaa kwa muda mrefu na tayari raia walikuwa wameshafika na kuharibu eneo.
Wakili: Je, hukuweza kumshirikisha mtu katika shughuli hiyo?
Shahidi: Hapana kwa sababu Jeshi la Polisi halisemi uongo na tulikuwa chini ya kiapo
Wakili: Je, baada ya hapo ulienda wapi?
Shahidi: Nilikwenda katika Kituo cha Polisi Bomang’ombe na nililala mpaka asubuhi katika gari.
Wakili: Ulisema katika gari ulikuwa na dereva ambaye pia ni polisi, je, una uhakika gani kama hakusogeza vielelezo?
Shahidi: Hakusogeza nina uhakika.
Wakili: Ile briefcase ya marehemu ilienda wapi?
Shahidi: Siwezi kujua.
Wakili: Je, utakubalina na mimi kwamba briefcase ya marehemu mliondoka nayo kwa sababu ilikuwa na fedha?
Shahidi: Sijazungumza habari za briefcase maana sijui suala hilo.
Wakili: Je, marehemu alivuliwa nguo wapi?
Shahidi: Sikuwapo na sijui.
Wakili: Je, utakubaliana na mimi, kwamba risasi huwa inatoboa nguo, si ndiyo?
Shahidi: Ndiyo ni kweli.
Wakili: Je, hukuona umuhimu wa kuwa na hizo nguo?
Shahidi: Mimi siyo mpelelezi wa kesi.
Wakili: Je, wakati unakusanya vielelezo katika eneo la tukio, hukuona umuhimu wa kukusanya nguo za marehemu?
Shahidi: Sikuona umuhimu na pia sikuwapo wakati wakimvua hizo nguo.
Wakili: Je, ulipata ushahidi wa mtu aliyemvua nguo marehemu?
Shahidi: Hapana, kwa sababu sikuwapo
Wakili: Hivyo utakubaliana na mimi katika ukusanyaji wa vielelezo kuna baadhi ya vielelezo vilipotea?
Shahidi: Hapa sikubaliani na wewe.
Wakili: Je, ulikagua mifuko ya marehemu?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Je, hukukuta fedha au leseni ya udereva?
Shahidi: Hapana sikukuta kitu.
Wakili: Je, marehemu anawezaje akaendesha gari pasipo kuwa na leseni ya udereva?
Shahidi: Hapana, siwezi kujua.
Mbali na Wakili Safari kumuhoji shahidi huyo pia wakili Hudson Ndusyepo anayemtetea mshtakiwa wa kwanza ambaye ni Sharif Muhamed, alimhoji shahidi huyo na mahojiano yao yalikuwa hivi:
Wakili: Kama ulivyosema shughuli zako za upelelezi, moja ya jukumu lako jingine ni kukagua makosa ya jinani, je, ulishakagua mangapi?
Shahidi: Matukio ni mengi, siwezi kukumbuka.
Wakili: Katika hayo matukio mengi uliyokagua na kuchorea ramani yalikuwa ni mangapi?
Shahidi: Bado ni mengi.
Wakili: Je, ni zaidi ya 10?
Shahidi: Ndiyo, yanaweza kufika na zaidi
Wakili: Je, unaweza kusema ramani inakuwa ni kielelezo au nini?
Shahidi: Uchoraji wa ramani unasaidia kuonyesha uhalisia wa tukio.
Wakili: Ina maana yoyote?
Shahidi: Ndiyo, ina maana kwa sababu  inaelezea vielelezo vilivyookotwa kwa ajili ya kukamilisha ushahidi.
Wakili: Je, pale panapotokea utata wa ramani unaweza kusaidia mahakama kwenda hadi eneo la tukio kuonyesha vitu vilivyopo kwenye ramani?
Shahidi: Ndiyo, vingine unaweza kuonyesha na vingine usionyeshe.
Wakili: Ni vitu gani unaweza kuonyesha kwa mujibu wa ramani?
Shahidi: Ni vitu ambavyo haviharibiki.
Wakili: Ramani huwa ni siri au ni faida ya mahakama?
Shahidi: Siyo siri.
Wakili: Naomba nikurejeshe katika kielelezo cha P3 kilichotolewa na upande wa Jamhuri, je, umekiona?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Unafanya kazi kwa PGO 229, ni kweli au si kweli?
Shahidi: Ni kweli ila sina uhakika na kifungu namba hicho kwa sababu PGO ni kubwa.
Wakili: Je, Agosti mwaka 2013, kati yako na OC- CID wa Hai ambaye ni shahidi namba moja wa upande wa Jamhuri, wewe na yeye nani alikuwa wa kwanza kufika eneo la tukio?
Shahidi: Yeye ndiye alikuwa wa kwanza
Wakili: Yeye OC-CID anasema bastola aliikuta kwenye briefcase nyeusi na wewe unasema ilikuwa katika mwili wa marehemu, sasa hapo ni yupi mkweli?
Shahidi: Mahakama itaamua, lakini pia siwezi kumsemea shahidi maana sikuwapo.
Bilionea Msuya ambaye alikuwa mfanyabishara wa Madini ya Tanzanite, Arusha, aliuawa Agosti 7, mwaka 2013 kwa kupigwa risasi 22, saa sita mchana, kandokando ya barabara kuu ya Arusha kuelekea Moshi, jirani na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Kesi hiyo namba 12 ya mwaka 2014, inasikilizwa na Jaji Salma Maghimbi na inawakabili washitakiwa saba, ambao ni Sharifu Mohamed, Shaibu Said, Musa Mangu, Jalila Said, Sadik Jabiri, Karim Kihundwa na Ally Musa. Kesi hiyo, itaendelea leo.