MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba, amesema pamoja na baadhi ya watu kwenda kutoa matusi dhidi ya nchi nje ya mipaka ya Tanzania, lakini bado CCM itaendelea kulinda hostoria ya nchi na watu wake kwa gharama yoyote.
Kauli hiyo aliitoa juzi jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa shina la wakereketwa la Chidya lililopo Mtaa wa Kimamba Kata ya Makurumla jijini Dar es Salaa, ambapo alisema histoa ya Tanzania italindwa kama Ukawa wanaendelea kutoa lugha zilizokosa utu na uzalendo kwa nchi.
“Ni lazima tulinde historia ya Taifa letu hata kama Ukawa wao wanatukana huko kwa wakoloni waliotutawala. Na ifike mahali tulinde utu wetu, nchi hii sasa imefika wakati wa kuandika vitabu vidogo vya historia.
“TANU na baadaye CCM imepambana kulinda utu na uzalendo wa Taifa letu. Leo tupo hapa kwa sababu tu wapo wazee wetu abao walijitoa kwa sababu yetu nasi CCM tutalinda heshima hiyo kwa gharama yoyote,” alisema Kamba.
Mwenyekiti huyo wa CCM alipongeza kazi kubwa inayofanywa na serikali ya Awamu ya Tano ikiwamo kujenga miradi mikubwa ya maendeleo ikiwamo reli ya kisasa, barabara za njia nane Kimara-Kiluvya.
“Tunaona kazi kubwa inayofanywa na hii inatokana na Watanzania sasa kuelewa maana ya kulipa kodi zetu miradi inajengwa mingi katika jiji la Dar es Salaama mbalo ndilo kituvu kikuu cha biashara.
“Na sasa ni miaka mitatu ya Rais Magufuli tangu aingie madarakani hajaomba misaada kutoka mataifa ya nje na bado tunasimama kwa miguu yetu Watanzania tuendelee kumuunga mkono kwa hali na mali,” alisema.
Pamoja na hali hiyo alisema bado kumekuwa kuna kuimarishwa kwa huduma za afya ikiwamo ujenzi wa hospitali na vituo vya afya pamoja na kuweka dawa za kutosha huku akiwataka Watanzania kujenga utamaduni wa kukata bima za afya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ubungo, Lucas Mgonja, alisema katika kuadhimisha miaka 42 ya kuzaliwa CCM chama hicho kimeweza kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kujenga madarasa kwa shule mbalimbali.