Na RATIFA BARANYIKWA-DAR ES SALAAM Â
HII ni wiki ya kwanza tangu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iruhusu kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2020 kuanza huku vyama vitatu tu kati ya 15 ndivyo vinavyoonekana kusikika.
Vyama hivyo tayari vimezindua kampeni hali kadhalika ilani zao na wagombea wake wanaonekana kukata mbuga kunadi sera zao.
Vyama hivyo ni Chama Cha Mapinduzi (CCM),Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha ACT-Wazalendo ambavyo wagombea wake wakiwamo wale wa urais wa Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania wametawanyika katika maeneo mbalimbali nchini.
Chama cha ACT-Wazalendo ambacho miaka mitano iliyopita hakikuwa kwenye orodha ya vyama vitatu vinavyoonekana kuchuana, kinaonekana kuchukua nafasi ya Chama Cha Wananchi, CUF kinachojikongoja kutoka kwenye vidonda vya migogoro wa tangu baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Katika chaguzi takribani zote chini ya mfumo wa vyama vingi, kwa mara ya kwanza CUF inaonekana kukaa nje ya mchuano mkali kwa sababu ya vidonda vya mgogoro wa kiuongozi na nafasi hiyo imechukuliwa na ACT-Wazalendo.
Chama cha ACT-Wazalendo kinawaacha wengi katika maswali na mjadala wa jinsi kilivyoanzishwa na kukua kwa kasi huku waasisi wake karibu wote wakiwa wametimkia Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiwamo mgombea wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Anna Mghwira ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Jabali la siasa za upinzani Visiwani Zanzibar aliyekibeba CUF kwa takribani miaka 29 zaidi kwa mbeleko imara na hata kufanikiwa kukitikisa CCM kwa miaka yote, Maalim Seif Sharif Hamad yupo ACT – Wazalendo yeye na wenzake ndio wanaoonekana kukipa nguvu chama hicho katika kampeni hizi mbele ya CUF.
Hata Maalim Seif na timu yake kwenda ACT-Wazalendo na si Chadema chama walichoshirikiana vyema katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, bado uamuzi huo umeendelea kuleta taswira yake katika wakati huu wa kampeni ambapo vyama vya upinzani vinapambana dhidi ya CCM ambayo nayo imejaribu kukataa kutengeneza vidonda tena vilivyoigharimu huko nyuma kushika dola.
Maalim Seif yupo ACT-Wazalendo baada ya mgogoro mkubwa wa kikatiba na kiuongozi na Mwenyekiti wake Prof. Ibrahim Lipumba, uhasama ambao tangu mwanzo hata kabla ya kuanza kwa kampeni ulionekana wazi kukidhoofisha chama hicho.
Maalim Seif na timu yake iliyokuwa ikitikisa siasa za Zanzibar safari hii wameajipanga katika mazingira tofauti ya ACT- Wazalendo, chama ambacho hata katika uchaguzi wa mwaka 2015 hakikuwemo kwenye ushirika wa vyama vya upinzani ambao ulitikisa kura za urais wa Dk. Shein na nafasi nyingine visiwani humo.
Chama hicho katika uchaguzi wa 2015 kiliambulia mbunge mmoja tu.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, wakati ACT-Wazalendo ikijiweka kando, vyama vinane viliungana chini ya ubatizo wa Ukawa na kumsimamisha mgombea wa urais, Edward Lowassa aliyepata kura milioni 6.07, sawa na asilimia 39.97 huku Magufuli wa CCM akipata kura milioni 8.8 sawa na asilimia 58.47.
Mbali na nafasi ya urais, vyama hivyo viliachiana majimbo kulingana na mgombea ambaye alikuwa akikubalika zaidi katika eneo husika.
Uchaguzi huo wa mwaka 2015 uliohusisha majimbo 258 kati ya 264, CCM ilishinda ubunge katika majimbo 188, CUF 35, Chadema 34, NCCR–Mageuzi kiti kimoja. NLD haikupata kiti wakati ACT – Wazalendo ilipata kiti kimoja kilichochukuliwa na Zitto Kabwe kupitia jimbo la Kigoma Mjini.
Kwa hesabu hiyo, Chadema ilifikisha wabunge 70 kutoka 48 wa mwaka 2010, CUF ilipata wabunge 45 kutoka 36 wa mwaka 2010 wakati NCCR-Mageuzi ikishuka kutoka wabunge wanne wa 2010 hadi mmoja na kufanya idadi ya wabunge wa Ukawa kuwa jumla 116 na CCM ikifikisha wabunge 252.
Idadi hiyo ya wabunge wa upinzani ndiyo kubwa kuwahi kufikiwa na upinzani tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na baadaye kufanyika uchaguzi wa kwanza wa ushindani mwaka 1995.
Muungano huo wa vyama vya upinzani mwaka 2015 ambao ulibebwa na nguvu Muungano huo na vigogo wa siasa za upinzani hasa kwa upande wa visiwani Zanzibar, Maalim Seif na timu yake, kama akina Babu Duni Haji, Ismail Jussa na wengine visiwani humo ulikuwa ni wa vyama vya CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD.
Ukiacha CUF, vyama vingine vilivyokuwa vimeingia katika muungano huo havikuwahi kuwa na nguvu ya kufurukuta visiwani humo kama ilivyo kuwa kwa CUF ya Maalim Seif.
Kilichotokea mwaka 2015 na hata Tume ya Uchaguzi (ZEC) iliyokuwa chini ya Jecha Salum Jecha kulazimika ama kupenda au kutopenda kuitisha uchaguzi wa marudio, ni nguvu ya CUF iliyokuwa ikibebwa na Maalim Seif na timu yake ambayo sasa ipo ACT-Wazalendo.
Chama cha ACT-Wazalendo kinachoongozwa na mwanasiasa kijana machachari, Zitto Kabwe ni cha tatu kwa Maalim Seif kujiunga nacho tangu alipoingia kwenye siasa.
Wakati kampeni zikionekana kusikika zaidi zile za vyama vitatu wagombea urais wengine wawili wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashimu Rungwe na Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba wameanza kutoa ahadi.
Wakati mwelekeo wa kampeni za CUF ukionekana kupwaya katika wiki ya kwanza, wengi wanasubiri kuona kama katika siku zaidi ya 50 zilizobaki kitakuja na kasi ile ile.
Jana mgombea wa Chaumma, Rungwe ambaye amebeba sera ya ‘kula ubwabwa na kuku bure’ ambayo tayari Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa imepiga marufuku ikisema kuwa ni kosa la kutoa rushwa alizindua kampeni zake, Manzese, Dar es Salaam.
Kilichokuwa kikivuta, kufurahisha, kuwaacha wengi kwenye vicheko na kumwongezea umaarufu ni huo ubwabwa wake uliopigwa marufuku.
Rungwe ambaye aliamua kuja na sera ambayo si ya kawaida ya kutoa ubwabwa na kuku bure kila siku isipokuwa Ijumaa siku ya biriani ghafla aligeuka mjadala mkubwa huku wengi wakifanya utani kwenye mitandao ya kijamii.
Mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli aliyezindua kampeni zake Dodoma Jumamosi iliyopita, Tundu Lissu wa Chadema aliyezindua kampeni Zakhiem-Mbagala Ijumaa iliyopita na Bernard Membe wa ACT-Wazalendo aliyeanzia Lindi wanaendelea kuchanja mbuga katika maeneo mbalimbali nchini kunadi sera zao.
Mambo makubwa ambayo yamegusa kampeni zao wagombea hao ni suala zima la miundombinu, ajira, mishahara, elimu, haki.
Ratiba ya awali ilikuwa inaonyeha kuwa CUF ilikuwa izindue kampeni zake Septemba 3 Mtwara.
UPDP kwa upande wake ilisema itazindua kampeni zake Lindi Septemba 19.
SAU nayo ilisema itazindua kampeni zake jijini Dar es Saalaam Septemba 3, NCCR- Mageuzi ilisema ingezindua Septemba 5, Dar es salaam DP Septemba 15.
AAFP ilisema ingezindua Septemba 5 Pwani pia ADC waliahidi kuzindua Kigoma Septemba 9 na vyama vingine NRA, NLD na ADA-Tadea bado vilikuwa vinajipanga.