Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KAMANDA wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleimani Kova, ameongezewa muda wa kustaafu kwa lengo la kupisha uchaguzi wa mwaka 2015.
Habari za uhakika ambazo MTANZANIA ilizipata mjini Dar es Salaam jana kutoka kwa mtu wa karibu na Kamanda Kova, zinasema alitakiwa kustaafu Juni 26, mwaka huu kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma.
“Kamanda Kova ameongezewa muda wa kustaafu hadi mwakani, lengo ni kupisha uchaguzi mkuu ujao na baada ya uchaguzi huo kupita ndipo atakapostaafu rasmi,” alisema.
Kustaafu kwa Kamanda Kova kulikuwa kunaenda sambamba na kustaafu kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Marietha Minangi, ambaye tayari amestaafu.
Baada ya Kamanda Minangi kustaafu, nafasi yake imechukuliwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi, Merry Nzuki.
“Baada ya Kamanda Minangi kustaafu aliyeshika nafasi yake sasa ni Kamanda Nzuki na tayari ameanza kazi ingawa hajatambulishwa rasmi,” kilisema chanzo chetu.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa kumekuwapo na mabadiliko kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Englibert Kiondo ambaye amehamishiwa makao makuu.
Habari za kuaminika zinasema Kamanda Kiondo muda wowote atakabidhi ofisi hiyo kwa kamanda mwingine ambaye bado jina lake halijawekwa hadharani.
“Mabadiliko yaliyofanywa na jeshi hili ni kwamba, Kamanda Kiondo anahamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani ila sijapata jina kamili la kamanda atakayeshika nafasi yake kwa sababu hajawekwa hadharani,” alisema.
Kamanda Kova alichukua nafasi ya Kamanda Alfred Tibaigana ambaye alistaafu kwa mujibu wa sheria.
Alipoulizwa kuhusiana na taarifa hizo, Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, Advera Senso, hakukataa wala kukubali zaidi ya kusisitiza kuwa mambo yanayohusu masuala ya ajira ni siri ya mwajiriwa na mwajiri wake.
“Kova ni mwajiriwa wa Serikali kwa taratibu za kazi ni masuala ya watu wawili kati ya mwajiri na mwajiriwa.