Veronica Simba na Zuena, Msuya
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imetoa wito kwa Serikali kuwa wakandarasi ambao hawakutekeleza miradi ya umeme vijijini kwa kiwango kinachoridhisha katika awamu zilizopita, wasipewe tena kazi hiyo.
Wito huo ulitolewa jana, Mei 31, 2021 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dustan Kitandula alipokuwa akitoa majumuisho ya hoja mbalimbali zilizotolewa na baadhi ya Wajumbe, katika semina iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati, ikilenga kuijengea Kamati hiyo uelewa wa kazi zinazoendelea kutekelezwa na sekta husika.
Alisema, baadhi ya wakandarasi wamekuwa wakikwamisha jitihada na dhamira njema ya serikali inayolenga kuwafikishia umeme wananchi wote walioko vijijini, kutokana na kuchelewesha kukamilisha miradi hiyo na wengine kutekeleza chini ya kiwango kinyume na mikataba yao.
Aliutaka Uongozi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake, hususan Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kutoa kipaumbele kwa wakandarasi waliotekeleza kazi zao kwa umahiri katika awamu zilizopita.
Akizungumza kwa niaba ya Uongozi mzima wa Wizara na Taasisi zake, Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani aliwahakikishia Wajumbe wa Kamati hiyo kuwa, Serikali itazingatia maelekezo yote yaliyotolewa.
Akifafanua, Waziri Kalemani alieleza kuwa tayari Serikali ilikwishachukua hatua za kuachana na wakandarasi wabovu ambapo alibainisha kuwa katika utekelezaji wa mradi wa usambazaji umeme vijijini, awamu ya tatu, mzunguko wa pili ambao unaendelea hivi sasa, wakandarasi wote wazembe hawakupewa kazi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kalemani aliieleza Kamati hiyo kuwa, Wizara yake imeamua kutumia nguzo za zege katika maeneo korofi hususan yenye ardhi inayohifadhi maji ili kutatua changamoto ya kuharibika kwa nguzo za miti ndani ya kipindi kifupi.
Pia, aliahidi kuwa Wizara ya Nishati itaendelea kusimamia kikamilifu suala la uzalishaji nguzo za miti zenye ubora, unaofanyika ndani ya nchi ili kuhakikisha zinakidhi viwango vya kimataifa.
Aliongeza kuwa, lengo ni kuepusha hasara katika miradi ya usambazaji umeme inayotekelezwa kote nchini, ambapo Serikali inatumia nguzo hizo baada ya kuacha kuagiza kutoka nje ya nchi.
Awali, akiwasilisha mada kuhusu miradi mbalimbali inayotekelezwa na REA, Mkurugenzi wake Mkuu, Mhandisi Amos Maganga alibainisha kuwa Wakala umejiwekea malengo ya kufikisha miundombinu ya umeme kwenye vijiji vyote Tanzania Bara, ifikapo Desemba, 2022.
Aidha, alieleza kuwa REA imejipanga kuhakikisha hali ya upatikanaji wa huduma za umeme inafikia asilimia 100 ifikapo mwaka 2030.
Kwa upande wa mafanikio, Mhandisi Maganga alibainisha kuwa ni pamoja na kufikisha na kusambaza umeme katika Makao Makuu ya Wilaya zote za Tanzania Bara. Vilevile alisema, kupitia REA, Serikali imewezesha hali ya upatikanaji wa umeme maeneo ya vijijini kuongezeka kutoka asilimia mbili mwaka 2007 hadi kufikia asilimia 69.6 mwaka 2020.
Alitaja mafanikio mengine kuwa ni kuwezesha taasisi za afya, elimu na maji kufikiwa na huduma za umeme hivyo kuboresha na kuongeza ufanisi katika utoaji huduma. Pia, kuwezesha uboreshwaji wa kilimo cha umwagiliaji katika mashamba.
Semina hiyo ilifanyika katika Ofisi ndogo za Wizara zilizopo Kikuyu Dodoma.
Viongozi wengine wa Serikali walioshiriki ni pamoja na Naibu Waziri wa Nishati Stephen Byabato, Katibu Mkuu Mhandisi Leonard Masanja, Naibu Katibu Mkuu Kheri Mahimbali na Wataalamu mbalimbali wa Wizara, REA na TANESCO.
Taasisi nyingine zilizowasilisha mada katika semina hiyo ni kutoka TANESCO iliyowasilishwa na Mkurugenzi wake Mtendaji, Dkt. Tito Mwinuka pamoja na kampuni yake tanzu ya uendelezaji jotoardhi (Tanzania Geothermal Development Company – TGDC), iliyowasilishwa na Meneja Mkuu, Mhandisi Kato Kabaka.