Na Esther Mnyika, Pwani
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imesema imeridhishwa na utekelezaji wa mradi wa kituo cha kupoza umeme cha Chalinze ambao umefikia asilimia 93.7 huku njia ya kusafirisha umeme kutoka Bwawa la Julius Nyerere kuja Chalinze ikifikia asilimia 99.5.
Akizungumza Mei 18,2024 baada ya kukagua mradi huo unaosafirisha umeme unaozalishwa kutoka Bwawa la Julius Nyerere-(JNHPP) hadi kituo cha kupoza umeme cha Chalinze Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Kirumbe Ng’enda amesema kukamilika kwa mradi huo utachochea sera ya nchi ya uchumi wa viwanda kwa kuwa hakuna maendeleo ya viwanda pasipokuwa na umeme wa uhakika.
Amemesema wameridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi wa kituo cha kupoza umeme cha Chalinze unaojumuisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 400 kutoka JNHPP hadi Chalinze.
“Tunampongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kwa kuendelea kutekeleza miradi ya nishati, kasi ya ujenzi wa mradi huu imeongezeka kutoka asilimia 55 ya mwaka jana na kufikia asilimia 93.7 mwaka huu,” amesema Kirumbe.
Amesema Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imefanya kazi kubwa katika kutekeleza mradi huo ambapo ujenzi wa jengo la mitambo umekamilika kwa asilimia 100 na kukamilika kwa utekelezaji wa mradi huo utazidi kuimarisha hali upatikanaji wa umeme wa nchini na mwingine kuuzwa nje ya nchi pale mahitaji yanapotosheleza.
Naye Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema miradi hiyo ambayo iko ukingoni kumalizika ilianza mwaka 2021 chini ya uongozi wa Rasi Dk. Samia Suluhu Hassan ambayo tija yake imeonekana baada ya changamoto ya upatikanaji wa umeme kupungua kutokana na kuanza kutumia umeme kutoka bwawa la Julius Nyerere.
Aidha, amewashukuru Wajumbe wa Kamati hiyo kwa ufuatiliaji na ukaguzi wa mradi huo ambao una maslahi mapana kwa Taifa zima na kuahidi kuendelea kuyafanyia kazi maelekezo yanayotolewa na wajumbe hao.
“Mradi huu umegharamiwa na serikali kwa asilimia 100 na gharama ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ni shilingi bilioni 158 ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 99.5. Pia gharama ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Chalinze ni shilingi bilioni 128 ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 93.7,” amesema Kapinga.
Amesema kwa sasa wanakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa miundombinu ikiboreshwa watapata umeme wa uhakika.
Kwa upande wake Meneja wa mradi wa kituo cha kupoza umeme cha Chalinze, Mhandisi Newton Livingstone Mwakifwamba amesema kukamilika kwa mradi wa kituo hicho utasaidia kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme na kuimarisha miundombinu wezeshi ya kupokea Umeme na kuingiza kwenye Gridi ya Taifa.
Amesema ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Chalinze ulianza Oktoba 2021 na unatarajiwa kukamilika Agosti mwaka huu gharama yake ni shilingi bilioni 128
na utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 93.7.
“Ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka JNHPP hadi Chalinze ulianza utekelezaji Julai, 2021 na unatarajiwa kukamilika Juni mwaka huu na grama yeke ni shilingi bilioni 158 utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 99.5 ambapo kwa sasa njia zote mbili za kusafirisha umeme zimewashwa na zinapitisha megawati 235 za mashine namba 9 kutoka Bwawa la JNHPP kuja Chalinze,” amesema Mhandisi Mwakifwamba.