BENJAMIN MASESE Na FATUMA SAID-MWANZA
ALIYEKUWA Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza (RPC), Jonathan Shanna, amesema wapinzani ni watu wazuri ndiyo maana katika muda wote aliokuwa bosi wa polisi kwenye mkoa huo, hawakuwahi kurushiwa mabomu na jeshi hilo.
Kamanda Shana ambaye kwa sasa amehamishiwa Makao Makuu Kitengo cha Operesheni, aliyasema hayo jana wakati akimkabidhi ofisi Jumanne Muliro ambaye ndiyo RPC mpya wa Mkoa wa Mwanza.
Alisema kati ya vitu anavyojivunia katika uongozi wake ni kutolalamikiwa ama yeye kuwalalamikia viongozi wa vyama vya siasa na waandishi wa habari ambao kwa pamoja walimpa ushirikiano wa karibu na kupata taarifa nyeti.
Shanna alisema viongozi wa siasa hasa wapinzani, wanachukuliwa ni watu wa vurugu lakini alisisitiza ni watu wazuri unaposhirikishana jambo na kukubaliana.
Alisema hakuna haja ya kurushiana mabomu kwa sababu yeye tangu aingie Mkoa wa Mwanza haijawahi kutokea bomu likarushwa kwa wanasiasa, bodaboda, machinga wala watu wengine.
“Kutoka moyoni kwangu na nayasema maneno hayo kwa dhati bila unafiki, viongozi wa vyama vya siasa na waandishi wa habari mkoa huu ni watu ambao wamenipa ushirikiano mkubwa sana, kama ni taarifa nimezipata huko na nilipokuwa nazifuatilia nakuta zina ukweli.
“Kama ni waandishi wanaoandika habari za kweli zilizojitosheleza kwa kila upande ‘balanced’ ni hapa Mwanza, natamani wengine waje kujifunza.
“Kwanza ukiwaita muda wowote wanafika na tunakwenda wote kwenye mapango, vile vile viongozi wa dini nao hawako nyuma wamesaidia mkoa kuwa na amani.
“Nimeondoka hapa nikiwa salama sijaondolewa hata cheo kimoja kama mnavyoona hapa begani, hii inatokana na ushirikiano na maofisa wenzangu wa polisi na kamati za ulinzi.
“Tangu nije Mwanza haijawahi kutokea tunapiga mabomu bodaboda, machinga, madereva wa daladala au wananchi kwa sababu ya maandamanao au vurugu, hawa watu ni kukaa nao na kukubaliana nao,”alisema.
Hata hivyo alisema moja ya tukio ambalo hawezi kulisahahu ni ajali ya kivuko cha MV Nyerere kilichokuwa kikifanya safari zake kati ya Bugorola na Ukara Wilayani Ukerewe ambacho kilipinduka Septemba 20, mwaka jana na kusababisha abiria 230 na wengine 41 kuokolewa.
Alisema katika ajali hiyo aliweza kupata changamoto kadhaa ambako alishirikiana na kamati ya ulinzi ya mkoa kuhakikisha watu wanaokolewa wakiwa hai ingawa baadhi yao walifariki dunia.
Muliro na majambazi
Kwa upande wake Muliro, aliwataka majambazi wanaofanya uhalifu kwa kutumia silaha, kuandika wosia kabla ya kuingia mitaani.
Alisema miongoni mwa watu atakaowashughulikia kwa nguvu zote ni majambazi wanaotumia silaha kwa kupambana na polisi au kuhatarisha usalama wa watu.
“Kipaumbele changu ni kusimamia kuzuia uhalifu hasa wale wanaotumia silaha za moto, anayejua hiyo ndiyo shughuli yake (ujambazi) ni heri akabadili mtazamo wake.
“Sitakubali kuona askari wangu anazuiwa na mtu anayejiita jambazi, huyo atabadilika jina lake kwanza, pia silaha yake inachukuliwa na pengine ndiyo itakayomshughulikia.
“ Nitatunza siri kwa watu wanaotoa siri na nitajenga misingi inayoongoza jeshi la polisi askari wafanye kazi kwa weledi, kama mtu yupo hapa anashirikiana na wahalifu ni vema wakashauriane kuacha biashara hiyo.
“Tangu nifike nimedokezwa na Shanna kwamba waandishi wa habari walimsaidia kupata taarifa nyeti, hivyo nami nitawatumia kufanikisha lengo langu,”alisema.