25 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

JUKWAA LA KATIBA LATAJA NJIA ZA KUDHIBITI WANASIASA KUHAMA VYAMA


PATRICIA KIMELEMETA NA TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM

Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) limependekeza yafanyike mabadiliko kwenye sheria ya uchaguzi   kudhibiti tabia ya wanasiasa kuhama vyao vyao na uchaguzi kurudiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari  Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Jukata, Hebron Mwakagenda, alisema mapendekezo hayo ni pamoja na kubadilisha vifungu vya sheria  kutomruhusu mwanasiasa aliyehama chama kwa hiari kugombea tena.

Alisema mwanachama atakayehama chama na kupoteza nafasi zake za kuchaguliwa, akae miaka 10 bila kugombea nafasi yoyote  kutoa nafasi kwa aliyemfuata wakati wa uchaguzi kuchukua nafasi yake.

“Mpaka uchaguzi wa Agosti 12 mwaka huu, Serikali imetumia Sh bilioni 15.8 kwa ajili ya kugharamia uchaguzi wa marudio wa wabunge na madiwani,”alisema Mwakagenda.

Alisema  katika uchaguzi huo, kata ndogo hutumia Sh milioni 20 huku kata kubwa hutumia Sh milioni 150 kwa kutegemea na wingi wa vituo na idadi ya wapiga kura.

Alisema kutokana na hali hiyo, fedha zinazotumika kwenye uchaguzi kama huo ni nyingi ambazo zingeweza kutumika kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mwakagenda alisema mapendekezo mengine ni pamoja na kutoa kinga kwa mwanasiasa atakayefukuzwa chama chake  aruhusiwe kubaki na nafasi yake kwa kuwa alichaguliwa na wananchi na siyo chama.

“Ikiwa mbunge au diwani amechaguliwa na wananchi lakini viongozi wa chama chake wamemfukuza, anapaswa kubaki na nafasi yake mpaka kipindi cha sheria cha kutumia nafasi hiyo kitakapoisha,”alisema.

Alisema ikiwa wanasiasa aliyechaguliwa na mwananchi kuwa kiongozi amefariki dunia, au ameshindwa kutekeleza majukumu yake kwa sababu za afya zilizothibitishwa na daktari, ndipo uchaguzi mdogo ufanyike.

Alisema ili kuhakikisha mapendekezo hayo yanafanyiwa kazi, Jukwaa  limedhamiria kuitisha mijadala ya taifa kwa ajili ya kuelimisha wananchi na viongozi wa serikali.

Alisema mpaka sasa   wamekwisha kuwasiliana na baadhi ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wa vyama vya upinzani  kuangalia namna ya kuwasilisha hoja binafsi katika kikao cha Bunge cha Novemba.

Aliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na polisi kutimiza majukumu yao  kwa mujibu wa sheria bila kuegemea upande wowote wa vyama vya siasa.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles