Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Baadhi ya wanawake wamesema kitendo cha wanaume kutotimiza wajibu wao na kukithiri kwa vitendo vya ukatili kunachangia kasi ya ongezeko la talaka.
Takwimu za mwaka 2020 za Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) zinaonyesha talaka 511 zilisajiliwa nchini na kati ya hizo 221 ni kutoka Dar es Salaam.
Aidha Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, wakati akizindua kituo jumuishi cha utoaji haki jijini Dodoma alisema kati ya mwaka 2017 hadi 2019 mashauri ya ndoa na talaka yalikuwa 4,200 na kwamba uamuzi wa kujenga mahakama jumuishi Temeke ulisukumwa na idadi kubwa ya mashauri ya mirathi, ndoa na talaka mkoani Dar es Salaam.
Wakizungumza wakati wa mjadala ulioandaliwa na Kikundi cha Sauti ya Jamii Kipunguni wamesema kukosa uwezo wa kiuchumi, athari za utandawazi, mfumo dume, wanaume kutotimiza wajibu wao na kukithiri kwa vitendo vya ukatili ndio sababu kubwa ya kuwapo kwa talaka.
Mjadala huo ambao uliwakutanisha wanawake na wanaume ulilenga kuzungumzia masuala ya familia ukijikita kujadili chanzo cha kuongezeka kwa talaka mkoani Dar es Salaam, athari zake na suluhisho.
“Mama anaamka asubuhi anakwenda kuuza mboga akirudi nyumbani watoto wanamlilia, mama ndiye anayetoa hela familia ile na baba akirudi anakuja kula ugali na matembele ambayo mama ametoka kutafuta.
“Lakini mama huyo huyo anapigwa kwa sababu anaonekana ni mzurulaji kwamba hajatoka kuuza mboga alikwenda kwenye mambo mengine,” amesema Beatrice Oswald mkazi wa Mzinga.
Naye Veronica Wana kutoka Kivule, amesema baadhi ya wanawake wamejisahau hali inayochangia waume zao kuchepuka.
“Sisi wenyewe wakati mwingine tukishaolewa tunajisahau, ulipoolewa ulikuwa msafi lakini dera la banda la kuku unaigia nalo ndani,” amesema Veronica.
Tabu Ally kutoka Majohe amesema kunatakiwa kuwepo na usawa baina ya mwanamke na mwanamume ndipo ndoa zitadumu.
Nao wanaume wamesema baadhi ya wanawake wamekuwa wakiwaonyesha dharau hali inayochangia ndoa kuvunjika.
“Mwanamume anatoka kazini ameshika hata kitabu unashindwa kumpokea, anaingia mpaka ndani umeshindwa kunyanyuka umekaa tu unapiga soga halafu mwisho wa siku lawama zinarudi kwa mwanamume,” amesema Nkemwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sauti ya Jamii, Selemani Bishagazi, amesema mjadala huo umehusisha viongozi wa vituo vya taarifa na maarifa kutoka maeneo ya Kisarawe, Temeke, Majohe, Kivule, Kitunda pamoja na wanajamii.
“Huwa tunakutana mara mbili kwa mwezi tunachagua mada ya kujadili, kama hili la takala tumejadiliana tunafanya nini kumaliza tatizo,” amesema Bishagazi.