RAIS Dk. John Magufuli anatarajia kuwa mwenyeji na mwenyekiti wa mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC unaotarajia kufanyika Agost 17 na 18, mwaka huu jijini Dar es Salaam
Rais Magufuli ambaye kwa sasa ni Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo alishika nafasi ya uenyekiti wa SADC Agost mwaka jana, katika mkutano uliofanyika Windhoek nchini Namibia nafasi ambayo ni ya mzunguko akiichukua kutoka kwa Rais wa nchi hiyo Dk. Hage Geingob na atahudumu kwa muda wa mwaka mmoja kuanzia Agosti 2019 hadi Agosti 2020.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema kwa sasa maandalizi ya mkutano huo yanaendelea kufanyika.
“Maandalizi ya maonesho na maadhimisho haya ya wiki ya viwanda yanaratibiwa na Wizara za Viwanda na Biashara pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje, ni adhimu na muhimu sana, nawaomba wafanyabiashara na wadau wote wajitokeze katika kushiriki maonesho haya ambayo yataleta tija ya masoko na viwanda kwenye nchi yetu,” alisema Profesa Kabudi.
Alisema hadi sasa tayari wajumbe sita kutoka katika Sekretarieti ya SADC wamewasili nchini kwa ajili ya maandalizi ya awali ya mikutano na maadhimisho hayo.
Akizungumzia maandalizi Naibu Katibu Mtendaji wa Sekretariat hiyo, Balozi Joseph Nourrice alisema lengo ni kuhakikisha wanafanikisha azma yao hiyo.
“Sisi Sekretarieti tumekuja kufanya maandalizi ya mikutano hii kuanzia ngazi ya maofisa, mawaziri, makatibu wakuu na wakuu wa nchi na Serikali zao, tuna hakika tutafanikisha jambo hili,” alisema Balozi Nouricce
Mwenyekiti wa sasa wa SADC Rais Dk. Magufuli atashirikiana na Sekretariat ya SADC katika kusimamia utekelezaji wa shughuli zote za kikanda pamoja na kuratibu na kusimamia mikutano mbalimbali ya kisekta kwenye nchi hizo.
Kwa mara ya mwisho mkutano wa SADC ulifanyika Tanzania mwaka 2013 ukiwa chini ya uenyekiti wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa ambapo kwa sasa ina nchi 16 wanachama zikiwepo za Tanzania, Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Jamhuri ya Visiwa vya Comoro, Falme ya Eswatini, Falme ya Lesotho, Namibia, Shelisheli, Afrika Kusini, Malawi, Msumbiji, Mauritius, Zambia, Zimbabwe na Madagascar.