Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
SIKU moja baada ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, kuandika barua ya kujiuzulu nafasi yake, hatimaye Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Dk. John Magufuli ameridhia kujiuzulu kwake.
Rais Magufuli aliridhia uamuzi huo wa Kinana kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), kilichofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam jana.
Akizungumza jana mbele ya wajumbe wa NEC, Rais Magufuli alisema ameruhusu na kuridhia mwanasiasa huyo amalize muda wake ili wamtafute katibu mkuu mwingine mpya.
“Huyu kweli ameshaomba zaidi ya mara mbili na zile zingine alikuwa anaomba kisirisiri nilikuwa namkatalia, akiweka neno hilo namwanzishia point (hoja) nyingine.
“Lakini nikatambua pia juhudi kubwa kwa kujiuliza kwamba ni makatibu wakuu wangapi wamekuwa CCM tangu tupate uhuru, nikajua kwamba walikuwepo hata wengine mimi bado sijaanza shule ya msingi na kila mmoja alifanya kazi yake na akamaliza wakati wake.
“Lakini nikatambua kuwa umri wa Kinana pia, nikamwita mzee Shein (Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais Dk. Ali Mohamed Shein), akasema kweli mkubalie, nikamwuliza Mangula (Makamu Mwenyekiti Bara, Philip Mangula) naye akasema haya tumkubalie.
“Nikaona nimwite tena jana (juzi) labda atakuwa amebadilisha mawazo, nikamwambia mimi nataka nibadilishe uendelee tu akasema hapana, naomba uniruhusu.
“Na mimi nimeridhika na nimejiridhisha na dhamira yangu ya moyo kwa kazi kubwa aliyoifanya ndugu yetu, lakini ukweli nimeridhia nimkubalie amalize muda wake wa ukatibu mkuu, tumtafute katibu mkuu mwingine,”alisema Rais Maguli.
Hatua ya kujizulu kwa Kinana imekuja baada ya MTANZANIA kuripoti taarifa hiyo isiyokuwa na shaka ambapo imeridhiwa rasmi na Rais Magufuli.
Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.