NA WAANDISHI WETU-DAR/MWANZA
RAIS Dk. John Magufuli, amepindua hoja ya kuvunjwa kwa Katiba baada ya kumteua Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Dk. Abdallah Possi kuwa balozi.
Uamuzi huo wa Rais Magufuli, umekuja huku kukiwa na mjadala mpana wa kudaiwa kuvunja Katiba kwa kuminya nafasi za uteuzi za wabunge wanawake.
Taarifa iliyotolewa jana usiku na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu wakati tunakwenda mitamboni, ilieleza kuwa kituo cha kazi na tarehe ya kuapishwa kwa balozi huyo mteule vitatangazwa baadaye.
Kabla ya uteuzi huo, Dk. Possi alikuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu aliyekuwa akishughulikia walemavu.
Kutokana na uteuzi huo, nafasi yake itajazwa baadaye.
Inaelezwa kuwa kutokana na uteuzi huo wa Dk. Possi, kuna hatari katika Bunge lijalo linaloanza vikao vyake Januari 31, huenda akajiuzulu ubunge ili kutoa nafasi ya uteuzi kwa mtu mwingine.
Ikiwa atafanya hivyo, wabunge wa kuteuliwa na Rais watabaki saba, wakiwamo wanawake wawili na wanaume watano.
Kwa hesabu hiyo, Rais Magufuli atabakiwa na nafasi tatu za uteuzi wa wabunge kutokana na nafasi 10 alizopewa kwa mujibu wa katiba.