29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

JPM AMGOMEA WAZIRI

DERICK MILTON, MEATU


RAIS Dk.John Magufuli amekataa ombi la Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ambaye pia ni Mbunge wa Kisesa mkoani Simiyu la kutaka jimbo lake liwe halmashauri.

Rais Dk.Magufuli alisema kuanzisha maeneo mapya ya utawala kumekuwa kukiongeza gharama za uendeshaji.

Alisema ni bora fedha hizo akazitumia kuwaletea wananchi maenedeleo kuliko kuongeza halmashauri.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana katika mji wa Mwandoya wilayani Meatu aliposimama kusalimia wananchi, wakati wa ziara ya kukagua shughuli za maendeleo.

Awali Mpina alimwomba Rais Dk. Magufuli kuwapatia halmashauri wananchi wa Kisesa kutokana na kutembea umbali mrefu kufuata huduma za kiutawala.

“Wananchi wa Kisesa wamekuwa wakipata wakati mgumu kwenda mji wa Mhanuzi ambapo kuna ofisi za halmashuari.

“Wilaya ya Meatu kuna majimbo mawili na yote yanategemea halmashauri moja. Hawa wananchi mheshimiwa Rais, wanatembea umbali wa kilomita zaidi ya 100 kwenda makao makuu ya mkoa, kilomita 60 kwenda makao makuu ya halmashauri.

“Mheshimiwa Rais umbali huo wote ni mrefu, sisi hatuombi wilaya, tunaomba utupatie halmashauri ya kwetu sisi wenyewe,” alisema waziri huyo.

Mpina alisema uwezo wa kujiendesha kama halmashauri upo, kutokana na kuwapo kwa idadi kubwa ya watu zaidi ya 170,000.

Alisema mbali na idadi ya watu, Jimbo la Kisesa lina uwezo wa mapato, kwani limekuwa likikusanya zaidi ya Sh bilioni 2 kwa mwaka pamoja na kuwapo kwa miundombinu mingine ya kutosha kuwa halmashauri.

Huku akishangiliwa na umati mkubwa wa wananchi, Waziri Mpina alisema kupatikana kwa halmashauri kutasababisha wananchi wa jimbo hilo kupata maendeleo kwa haraka.

JPM

Akizungumzia ombi hilo, Rais Magufuli alisema kwa sasa hawezi kuanzisha maeneo mapya wakati wananchi wengi bado ni maskini na badala yake atahakikisha anawaletea maendeleo na si kuwaletea halmashauri.

Rais Magufuli alilazimika kutoa mifano mbalimbali ya majimbo yenye maeneo makubwa, lakini kuna halmashauri moja, ambapo alitolea mfano wa halmashauri ya Chato ambayo alieleza kuwa idadi ya watu ni zaidi ya 400,000.

“Kuna majimbo mengi tena makubwa zaidi ya hili na yana idadi kubwa ya watu kuliko hapa Kisesa, kuna halmashauri moja, siwezi kuleta halmashauri wakati najua itaongeza gharama za uendeshaji,” alisema Rais Magufuli.

“Kupanga ni kuchagua, niache nishughulikie masuala ya barabara, umeme, maji na afya, siyo kuwaletea halmashauri, haya maombi yenu yatakuwa baadaye lakini siyo sasa hivi, siwezi kuleta halmashauri, nitaleta maendeleo,”alisema Rais Maguli.

Alisema hawezi kuwadanganya kuwa atawapatia  halmashauri wakati jambo hilo hawezi kulifanya kwa sasa.

Apinga uzazi wa mpango

Wakati huo huo, Rais Magufuli alisema hakubaliani na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalim, ambaye anapenda kuzungumzia uzazi wa mpango kwani anapunguza nguvu kazi ya Taifa.

“Nawaeleza ukweli mtandanganyika na mipango mingine ya ajabu sana, tunachotakiwa Watanzania ni kuchapa kazi ili watoto utakaowazaa uwalishe,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema kama mtu hawezi kufanya kazi halafu anakimbilia kwenye uzazi wa mpango anajidanganya. “Kama anaweza kulima shamba na ana miliki ng’ombe wa maziwa hakuna haja ya kupanga uzazi.

“Ninawaambia hayo ndio mawazo yangu, wale ambao hawafanyi kazi wavivu wavivu ndio wanajipangia watoto, analima mwaka mzima anategemea mnazi mmoja, saa zingine hata uzazi unakataa tu huwezi kuzaa kama una njaa,” alisema Dk. Magufuli.

Huduma

Rais Magufuli alisema Serikali yake itahakikisha inaboresha utoaji wa huduma za afya kwa kuongeza ujenzi wa vituo vya afya ili kuimarisha utoaji wa huduma hiyo kwa wananchi.

‘’Tutajenga hospitali za wilaya 67 nchi nzima ili kuwasogezea huduma wananchi, watumishi wa afya endeleeni kufanya kazi kwa bidii, nathamini taaluma zenu, mnafanya kazi za uponyaji…lakini madai yenu mengine tunaendelea kuyafanyia kazi’’ alisema Rais Magufuli.

Alitoa mwezi mmoja kwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleiman Jaffo kutafuta mkandarasi mara moja na kuanza ujenzi wa barabara za mji wa Mhanuzi kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita tatu, ambapo aliahidi kuzijenga tangu akiwa Waziri wa Ujenzi.

Alimtaka waziri huyo bila kujali kama atakuwa na bajeti hiyo kutekeleza agizo hilo mara moja kupitia Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA).

”Haiwezekani nitoe ahadi ya ujenzi wa barabara tangu nikiwa Waziri wa Ujenzi , mpaka sasa ahadi haijatekelezwa…yaani huu ni uzembe mkubwa  hakikisheni barabara zinaisha ndani ya kwaka huu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles