Na Aziza Masoud
-Dar es Salaam
RAIS Dk. John Magufuli, ametoa wito kwa Jeshi la Wananchi nchini (JWTZ) kupitia shirika lake la Nyumbu, kutengeneza magari ya zimamoto kama ambavyo shirika hilo limewahi kufanya katika miaka ya nyuma ili nchi iondokane na gharama kubwa zinazotumika kuyaagiza kutoka nje ya nchi.
Dk. Magufuli ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, alitoa kauli hiyo jana Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na majenerali, maofisa, askari na wageni waalikwa baada ya hafla ya kuwatunuku kamisheni maofisa wanafunzi 146 wa JWTZ kundi la 65/18 cheo cha Luteni Usu ambao kati yao wanaume ni 140 na wanawake sita waliomaliza mafunzo katika Chuo cha Kijeshi cha Monduli (TMA) kilichopo Arusha.
Pamoja na kutoa wito huo, Dk. Magufuli, ameeleza kuridhishwa kwake na kazi nzuri za kijamii zilizofanywa na JWTZ zikiwemo ujenzi wa ukuta katika eneo la madini ya Tanzanite mkoani Manyara ambayo ilifanyika kwa kipindi cha miezi mitatu.
Aidha, Dk. Magufuli, pia alitaja kazi nyingine zilizowahi kufanywa na JWTZ na kuridhishwa nazo ni uopoaji wa kivuko cha MV Nyerere kilichopata ajali katika Ziwa Victoria, uliotumia siku saba, ujenzi wa nyumba 41 katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma kwa miezi miwili na kukusanya korosho za wakulima katika msimu uliopita.
Ameliahidi Jeshi hilo kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha linajiimarisha katika majukumu yake yote na ametoa wito kwa maofisa wapya kutambua kuwa wapo katika Jeshi linaloheshimika na hivyo wanao wajibu wa kuhakikisha wanaendeleza sifa hiyo njema.
Naye Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo, alimshukuru Rais kwa kuendelea kuliamini, kutoa kipaumbele na kulitumia JWTZ katika majukumu mbalimbali ya kuwahudumia wananchi na ameahidi kuwa Jeshi hilo litaendelea kutimiza wajibu wake kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu ikiwa ni pamoja na majukumu ya kijamii.
Rais Magufuli alitunuku kamisheni kwa wanafunzi hao 146 ambao miongoni mwao wamo maofisa wanafunzi wanne ambao walipata mafunzo yao kutoka nchi rafiki, wawili Kenya na wawili Msumbiji.
Kabla ya tukio hilo alianza kwa kukagua gwaride lililoandaliwa na maofisa wanafunzi chini ya usimamizi wa Kaimu Mkufunzi Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli Arusha, Luteni Kanali William Lovukenya.
Baada ya gwaride hilo, Dk. Magufuli, alitoa zawadi kwa maofisa wanafunzi waliofanya vizuri wakati wa mafunzo ambapo maofisa waliopata zawadi ni pamoja na Frank Thadeo ambaye ni mshindi wa jumla katika fani zote, ofisa mwanafunzi, Beny Kalenga, ambaye ni mshindi katika taaluma na ofisa mwanafunzi, Josephine Mwambashi, ambaye aliibuka na ushindi wa jumla kwa wanawake.
Akitoa taarifa fupi ya mafunzo ya wanafunzi wa kundi la 65/18, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli, Brigedia Jenerali Stephen Mnkande, alisema maofisa hao wapya walianza mafunzo Machi 2018, wakiwa wanafunzi 236 ambapo kati yao 94 wameshindwa kufuzu kutokana na sababu mbalimbali.
“Wanafunzi 236 walioripoti chuoni Monduli ambapo kati yao wanaume walikuwa 227 na wanawake walikuwa tisa, lakini wanafunzi 94 walishindwa kuendelea na mafunzo kutokana na sababu mbalimbali na kwamba 146 waliofuzu wamefundishwa kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa na kukubalika kimataifa,” alisema Brigedia Jenerali Mnkande.
Alisema maofisa hao wapya waliotunukiwa Kamisheni katika cheo cha Luteni Usu wana viwango mbalimbali vya elimu ambapo Shahada ya Uzamili watatu, Shahada ya Kwanza 116, Shahada ya Juu watatu na 23 ni madaktari wa binadamu.
Sherehe za kuwatunuku Kamisheni maofisa hao zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda pamoja na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, makamanda mbalimbali wa JWTZ, wakuu wa majeshi na majenerali wastaafu, waambata wa jeshi kutoka nchi rafiki na wageni mbalimbali walioalikwa.