25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

URAIS MIAKA SABA: JPM AKATA MZIZI WA FITINA

Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli akizungumza na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa (CCM) Humphrey Polepole Ikulu jijini Dar es Salaam jana.PICHA : IKULU
NA MWANDISHI WETU - DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli amesema anasikitishwa na hafurahishwi na mjadala unaoendelea juu ya kuongezwa kipindi cha urais kutoka miaka mitano hadi saba kwa kuwa ni kinyume na Katiba ya nchi na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza Ikulu, Dar es Salaam jana alipokutana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Humphrey Polepole, Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, aliwataka wananchi kupuuza mjadala huo.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais – Ikulu, Gerson Msigwa, ilieleza kuwa katika mkutano huo Magufuli alimwelekeza Polepole kuwajulisha wanachama wa CCM na Watanzania kuwa anasikitishwa na hafurahishwi na mjadala unaoendelea juu kuongezwa kwa kipindi cha urais.

“Rais Magufuli amewataka wanachama wa CCM na umma wa Watanzania kwa ujumla kuupuuza mjadala huo kwa kuwa haujawahi kujadiliwa katika kikao chochote cha chama na ni kinyume na Katiba ya CCM na Katiba ya nchi,” alisema Polepole.

Polepole alisema Magufuli aliwataka wana CCM na umma wa Watanzania kutokubali kuyumbishwa ama kupotoshwa na mambo yasiyokuwa ya msingi, badala yake wajielekeze katika ajenda muhimu ya kujenga uchumi na kutekeleza Ilani ya CCM iliyonadiwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Pia alisema Magufuli hana mpango wowote na hatarajii kuongeza kipindi cha urais wakati wote wa uongozi wake.

Kauli ya Magufuli inajibu hoja za baadhi ya viongozi, wakiwamo wabunge ambao mara kadhaa walikaririwa wakitaka kuongezwa kwa ukomo wa urais na ubunge hadi kufikia miaka saba ili kumpatia rais na wabunge muda wa kutekeleza majukumu yao.

Hoja ya kuongeza ukomo wa urais ilianza kuibuliwa Septemba 12, mwaka jana na Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM), alipowasilisha kusudio lake la muswada binafsi wa mabadiliko ya Katiba unaohusu kuongeza ukomo wa Bunge.

Nkamia aliwasilisha kusudio hilo kwa mujibu wa kanuni ya 81(2) ya kanuni za Bunge toleo la 2016, kupitia barua yake aliyoisaini Septemba 12, mwaka jana  iliyokuwa ikipendekeza kuongeza muda wa Bunge kutoka miaka mitano hadi saba na kupunguza muda wa uongozi wa vijiji kutoka miaka mitano hadi minne.

Hata hivyo, kupitia ujumbe mfupi aliouandika katika mtandao wa kijamii wa WhatsApp, Nkamia, aliamua kuondoa kusudio hilo baada ya kile alichodai kuwa ni majadiliano na maelekezo kutoka kwa viongozi wa juu wa CCM.

Mbali na andiko hilo, mwaka jana MTANZANIA Jumapili lilimtafuta Nkamia kupitia simu yake ya mkononi na kumuuliza kama ana sababu nyingine zaidi ya alizozitaja kupitia ujumbe huo mfupi na lini atakuwa tayari kuwasilisha tena muswada huo.

Katika majibu yake, alisema: “Naomba ibaki hivyo hivyo kama ilivyo katika meseji sina cha kuongeza, kuhusu ni lini nitapeleka tena, nayo subiri kwa sababu nimesema nimesitisha kwa muda, maana yake nitawasilisha tena nitakapokuwa tayari.”

Hoja ya Nkamia ilipingwa na wanasiasa wakongwe, akiwamo Spika mstaafu wa Bunge, Pius Msekwa na wasomi mbalimbali.

Akizungumza na Kituo cha Televisheni cha Azam, Septemba, mwaka jana, Msekwa, alisema CCM haiwezi kukubaliana na maoni ya kuongeza muda wa kiongozi yeyote kutoka kipindi cha miaka mitano kilichopo kwa mujibu wa Katiba ya sasa.

Pia alisema kwa uzoefu wake bungeni, anaona kuna tafakari nyingi zilizofanywa kabla ya taifa kuamua kipindi cha utawala kuwa miaka mitano na si vinginevyo.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alipozungumza Septemba, mwaka jana na MTANZANIA Jumapili, alimpinga Nkamia, huku akisema lengo lake lilikuwa ni kujipendekeza kwa Magufuli ili ampe uwaziri.

Mbali na Nkamia, mwingine aliyetoa hoja ya kuongeza muda wa ukomo wa nafasi ya rais, ni Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Steven Ngonyani maarufu kwa jina la Profesa Maji Marefu, aliyetaka Magufuli aongezewe miaka mingine 10 ya kuongoza ili atawale kwa miaka 20.

Maji Marefu alitoa kauli hiyo Agosti, mwaka jana wakati Magufuli alipokuwa akizundua kituo kipya cha mabasi katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe.

Mbali na hao, pia hoja hiyo iliibuka Desemba, mwaka jana kwenye mkutano wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ambako wajumbe walitoa ushauri wa kuongeza ukomo wa urais na kuwa miaka saba na kujibiwa na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Idd, kuwa suala hilo linajadilika.

Balozi Seif alidai kuwa suala hilo haliwezi kuathiri Katiba ya Tanzania.

Wakati hao wakitoa hoja ya kuongeza muda wa ukomo wa urais, Septemba 18, mwaka jana, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema), alisema anakusudia kuwasilisha bungeni hoja binafsi ili kupunguza muda wa viongozi kukaa madarakani kutoka miaka mitano na iwe minne kama Marekani ili kutoa nafasi kwa wananchi kuwa na uamuzi zaidi wa kuendesha nchi yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles