25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

JPM AIMULIKA BENKI YA WALIMU

Na ASHA BANI -DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli  amesema muda wowote kuanzia sasa kuna hatari ya kufutwa  Benki ya Walimu Tanzania kutokana na kusuasua na kuyumba mtaji wake hali inayosabishwa na viongozi.

Aliyasema  Dodoma jana, alipofungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ambao utakuwa ni pamoja  na uchaguzi wa viongozi wa chama hicho.

Rais alisema Tanzania ina  a benki 58 ikiwamo  ya Walimu lakini haijawanufaisha walimu  wanaochangia benki hiyo na badala yake kuwanufaisha wachache wasio walimu.

“Tujiulizeni mlioweka fedha zenu huko na kukatwa asilimia mbili kuchangia, zinakwenda wapi?  Kuna wajanja wajanja ambao  wanajinufaisha na benki hiyo sasa naifuta muda wowote kuanzia sasa, tayari nimeshawasiliana na Benki Kuu,’’alisema Rais Magufuli.

Alisema alitakiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa benki hiyo lakini hakufanya   hivyo baada ya kuona ripoti yake  haikuwa nzuri baada ya kuwasiliana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Hata hivyo alimrushia kijembe kiongozi wao aliyepita ambaye hakumtaja  jina, kwamba alikuwa si kiongozi mzuri na kwamba alishiriki  kutafuna mali za chama kiasi   kwamba alibadilika maumbile yake katika muda mfupi wa uongozi wake.

Pia aliwashutumu baadhi ya viongozi wa CWT kwa kujiingiza katika siasa huku akiwataka viongozi   watakaochaguliwa kuwa makini na kutoruhusu siasa ndani ya chama hicho.

Akijibu changamoto hizo kupitia risala yao iliyosomwa na Kaimu Katibu Mkuu wa CWT, Simon Edwin,  aliwaahidi walimu hao kulipa deni la Sh bilioni 25 endapo tu kutakuwa na uhakiki wa madeni hayo kama yapo sahihi au la.

Alisema hatafumbia macho kuona mwalimu akisaini fomu yenye deni kwa ulaghai, akisisitiza ni lazima atamkamata na kumchukulia hatua.

Rais alisema  sababu zilizokwamisha kulipa madeni hayo ni pamoja na  wafanyakazi hewa hata ndani ya  walimu.

Aliwahakikishia kuwa endapo watafanya hesabu zao sawa sawa na kusaini yupo tayari kuyapeleka madai hayo kwa waziri mkuu na wakapatiwa malipo yao mara moja.

Rais Magufuli alisema sekta ya elimu ni nyeti katika taifa   hivyo ni vema ikapewa kipaumbele cha pekee kwa sababu  ni ufunguo wa maisha.

Vilevile, alieleza mafanikio mbalimbali yaliyopatikana tangu kupatikana kwa uhuru mwaka 1961 hadi sasa katika sekta hiyo.

Alisema shule za msingi zilikuwa 301 nchi nzima lakini sasa zipo 17,379.

Shule ya sekondari zilikuwa 41 lakini kwa sasa zipo 4,817 huku vyuo vikuu kutoka kimoja hadi kufikia   48.

Alisema bila kuwa na walimu hata majengo yote ni bure hivyo serikali ya awamu ya tano itahakikisha inaangalia elimu inakua nchini.

Rais alisema kuna umuhimu wa kuwa na wigo mpana katika elimu na  serikali kwa mwaka imetumia   Sh bilioni 535 kwa ajili ya kutoa   elimu bure.

Alisema mpango wa elimu bure umeleta mafanikio makubwa ingawa umekuwa na changamoto za hapa na pale likiwamo la uhaba wa walimu, vyumba vya madarasa na madawati.

Dk. Magufuli alisema  juhudi zinafanyika kuhakikisha matatizo hayo yanakwisha.

“Nitahakikisha nasimamia na kushughulikia matatizo yote ya walimu kwa kuwa mimi mwenyewe ni mwalimu na mke wangu mwalimu pia   na huwa ananikumbusha mambo mengi ya changamoto za walimu … na huwa mjanja kweli kwa kuwa anajua wakati mzuri wa kunikumbusha, wakati wa chakula,’’alisema Rais Magufuli.

Alisema kutokana na kuona umuhimu wa walimu, viongozi wengi aliowaweka ni walimu.

Aliahidi  kuendelea na utaratibu wa serikali wa kutoa mafunzo kwa walimu ya mara kwa mara .

Rais Magufuli alisema kwa sasa anaona mwelekeo mzuri kwa viongozi wa CWT na kwamba wanafungua ukurasa mpya wa utendaji kati ya serikali na chama hicho.

Aliwatakia heri katika uchaguzi wao huku akiwasisitiza kutochagua viongozi kwa   rushwa ambayo anaipinga.

Alisema yeye anapambana na rushwa na amekwisha kuanza   na wenzake ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwakamata wanaotumia rushwa, bila kujali kama atabaki na mwanachama mmoja.

Awali, akisoma risala, Kaimu Katibu Mkuu wa CWT, Simon Edwin alitaja  changamoto zao kuwa ni pamoja na ukosefu wa ajira, kutopandishwa madaraja, kutolipwa madeni ya mishahara na posho    mbalimbali zikiwamo  za madaraka.

Alisema mpaka sasa CWT inaidai serikali   Sh bilioni 25 kutokana na madeni mbalimbali yasiyo  ya mshahara na mengine ya mshahara.

Changamoto nyingine ni uhaba wa  nyumba za walimu jambo linalowafanya  kupata taabu mahali kuishi.

“Hali ya uhaba wa nyumba za walimu ni mbaya, hata za kupanga ni shida,  hivyo tunapendekeza ujenzi upewe kipaumbele  mikoani kama ilivyo kwa Mkoa wa Dar es Salaam.

“Walimu pia tupatiwe mikopo isiyo na riba  tuweze kujenga sisi wenyewe,’’ alisema Edwin

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles