27.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

JONAS MKUDE ARUDISHWA STARS

Na MOHAMED KASSARA -DAR ES SALAAM

KIUNGO mkabaji wa Simba, Jonas Mkude, amerudishwa katika kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, kinachotarajiwa kuingia kambini kesho kujiandaa na mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Benin utakaochezwa Novemba 11.

Mkude anarudishwa kwenye kikosi hicho baada ya kukosekana kwa muda mrefu, ambapo mara ya mwisho kuwa kwenye kikosi hicho ilikuwa katika mchezo wa kufuzu kwa fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan), Stars ikitolewa na Rwanda.

Nahodha huyo wa zamani wa Simba pamoja na kiungo wa Singida United, Mudathir Yahya, wamepata nafasi hiyo baada ya kocha mkuu wa kikosi hicho, Salum Mayanga, kufanya marekebisho madogo ya kuwaondoa beki Erasto Nyoni na kiungo, Mzamiru Yassin.

Nyoni na Mzamiru wameondolewa kwenye kikosi hicho kutokana na kuwa katika adhabu ya kutumikia kadi nyekundu walizopewa katika mchezo uliopita dhidi ya Malawi, uliochezwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Katika hatua nyingine, kocha wa timu za Taifa za vijana kwa upande wa wanaume, Oscar Mirambo, ametangaza majina ya wachezaji 35 wa kikosi cha timu chini ya umri wa miaka 23, kitakachoingia kambini kuanzia Novemba 5 hadi 16, mwaka huu.

Kikosi hicho kitakuwa na kambi hiyo ya takribani siku 10 na kucheza michezo miwili ya kirafiki na timu za ligi kuu ili kuchuja na kubaki wachezaji 25 watakaounda kikosi hicho kinachokabiliwa na michezo ya kufuzu kwa michuano ya Olimpiki itakayofanyika Japan mwaka 2020.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mirambo alisema wameita wachezaji hao ambao wengi wanatoka katika timu za Ligi Kuu ili kujenga kikosi imara kwa ajili ya michezo hiyo ya kufuzu inayotarajiwa kuanza mwakani.

“Kikosi cha chini ya miaka 23 kinatarajia kuingia kambini kuanzia Novemba 5 hadi 16, mwaka huu, katika kambi hiyo tumepanga kucheza michezo miwili ya kirafiki na timu mbili zinazofanya vizuri kwenye Ligi Kuu ili tupate kipimo sahihi cha kuchuja wachezaji na kubaki na 25 ambao wataunda kikosi hicho.

“Tumeamua kuufanya mwaka huu kuwa wa mwisho katika kutengeneza vikosi vya timu mbalimbali za vijana, tunafanya skauti ili mwakani tuwe na timu kamili zitakazokuwa na majukumu mbalimbali bila kuingiza wachezaji wapya,” alisema Mirambo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles