NA MWANDISHI WETU,
HIPPOCRATES ni mwanafalsafa wa kwanza kutambua harufu mbaya ya pumzi inayoweza kuhusiana na maradhi katika miaka ya 400BC.
Katika ripoti iliyotolewa na jarida la wall street journal, madaktari walielezea teknolojia ya kuchunguza kemikali zinazopatikana katika pumzi.
Kutoka kwa harufu mbaya mdomoni kunaweza kuwa ni dalili ya magonjwa kama kisukari, saratani ya mapafu, figo kushindwa kufanya kazi, hii ni kwa sababu zinahusika katika kutoa uchafu.
Obesity; kituo cha afya cha Cedars-Sinai huko Los Angels waliona kuna uwezekano wa harufu ya hewa ya mtu inaweza kuwa na uhusiano na ‘obesity’.
Aidha utafiti uliofanywa mwaka 2012 uligundua kuwa watu wenye matatizo ya moyo wana harufu tofauti kabisa katika pumzi zao.
Hata hivyo, mara nyingi watu wananuka midomo kutokana na vyakula wanavyokula vyenye asili ya protini. Pia kutokuwa makini na usafi wa kinywa kama vile kusafisha kinywa vizuri ikiwamo ulimi, huchangia kuacha mabaki ya chakula ambayo huoza na kusababisha harufu mbaya.
Ni vigumu mtu kujijua kama ana harufu mbaya kwa sababu ya mazoea. Mtu wa aina hii anaweza kumsema mwenzie kwamba ananuka mdomo na kutojua kama na yeye ana tatizo hilo.
Njia moja wapo inayoweza kukusaidia kutambua kuwa mdomo wako unatoa harufu mbaya ni kulamba nyuma ya kiganja cha mkono na kunusa, wengine hupumua mbele ya kioo na kunusa. Pia unaweza kutumia kijiti cha kuchokonolea meno na kukinusa.
Kisayansi unaweza kutumia vifaa kama Halimeter, Gas Chromatography na Bana Test.
Ili kuepuka hali hii unachotakiwa kufanya ni kula vyakula vyenye afya na ambavyo wakati wa kuvila vinaweza kusafisha kinywa vizuri.
Safisha meno angalau mara mbili kwa siku, asubuhi na baada ya mlo wa usiku. Hii itasaidia kuondoa au kujikinga na tatizo hilo.
Madaktari wa kinywa wanashauri kutumia kisafisha ulimi kuondoa mabaki ya vyakula kwenye ulimi.
Pia unaweza kutafuna bazoka ili kuongeza kiasi cha mate kwenye kinywa kilichokauka.
Baadhi ya bazoka zina viungo vinavyoondoa harufu mbaya mdomoni na zingine husafisha kinywa na kuondoa bakteria wanaosababisha harufu mbaya. Pia unaweza kutumia dawa ya kusukutua mdomoni, kabla ya kulala usiku.
Hakikisha unakunywa maji ya kutosha kila siku angalau glasi mbili.
Mwone daktari wako ukiona una tatizo la harufu mbaya mdomoni.
Ni vema kuepuka kunuka mdomo kwani tatizo hili linaweza kuathiri uhusiano, si wa kimapenzi tu bali hata marafiki. Pia huondoa haiba ya kupendwa kwani hata unapozungumza wengi watakwepa kuongea moja kwa moja na wewe kwa sababu ya harufu mbaya inayotoka kinywani mwako.
Huu si ugonjwa wa kuambukiza hivyo huna sababu ya kuogopa pindi unapokutana na mtu wa aina hii.