RAIS wa China, Xi Jinping, ameliagiza Jeshi la Ukombozi la Watu wa China (PLA) kutuma wafanyakazi wa kitengo cha afya zaidi ya 2,600 kwa ajili ya kusaidia vita dhidi ya mlipuko wa virusi vya corona huko Wuhan nchini humo.
Uamuzi huo, umekuja katika wakati ambao kuna taarifa wafanyakazi sita wa afya kufariki kutokana na virusi hivyo nchini humo, huku zaidi ya 1,700 wakiambukizwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Ubalozi wa China nchini Tanzania, ujumbe huo wa wafanyakazi wa jeshi utafanya kazi chini ya Hospitali ya Huoshenan ambayo ni ya kwanza ya muda iliyoanzishwa.
“Wafanyakazi hao ambao ni agizo la Rais watashugulikia hospitali mbili katika mji wa Wuhan na watafanyakazi chini ya Hospitali ya Huoshenshan, ambayo ni hospitali ya kwanza ya muda iliyoanzishwa mapema mwezi huu wakati wa janga la Corona lilipozidi kushika kasi.
“Hadi kufikia jana Februari 14, Jeshi la Ukombozi lilikuwa limepeleka vikundi vitatu vya wafanyakazi zaidi ya 4,000 wa matibabu mjini Wuhan tangu kuzuka kwa janga hilo,” ilieleza taarifa hiyo.
Aidha, taarifa hiyo ilisema kuwa Februari 13, mwaka huu jumla ya kesi mpya 5,090 zilikuwa zimethibitishwa huku kesi 2,450 mpya zikiripotiwa China bara, pia watu 1,081 walikuwa meruhusiwa kurejea nyumbani baada ya kupona na watu 121 wakifariki dunia.
“Katika Jimbo la Hubei, jumla ya kesi 4,823 zilizothibitishwa ziliripotiwa Februari 13, ambapo watu 690 walipona na watu 116 walifariki. Hii inamaana kwamba karibu asilimia 95 ya kesi mpya zilizothibitishwa na asilimia 96 ya vifo vilitokea Hubei Februari 13.
“Hadi kufikia jana Februari 14, China bara kulikuwa na kesi 63,851 zilizoripotiwa ambapo kati ya hizo 6,723 wamepona na kuruhusiwa kutoka hospitalini, 1,380 walifariki dunia na 55,748 bado wanaendelea na matibabu,” ilieleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa, hadi jana kulikuwa na jumla ya kesi 10,109 zinazoshukiwa ambazo zilikuwa zinasubiri majibu ya vipimo nchini China Bara na katika maeneo ya Hong Kong, Macao na Taiwan kulikuwa na kesi 71 zilizothibitishwa kuripotiwa na kifo kimoja huko Hong Kong.
“Katika jimbo la Hubei, jumla ya kesi 51,986 zilithibitishwa na vifo 1,318 vimeripotiwa jana sawa na asilimia 81 na asilimia 96 ya idadi yote ya China Bara.
“Utambuzi na mpango wa matibabu uliotolewa na Tume ya Kitaifa ya Afya ya China, kesi zote za homa ya mapafu zinazoshukiwa kupitia (CT) scan huhesabiwa kama kesi za vipimo vya kliniki,” ilieleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa, Tume ya afya ya jimbo la Hubei imesema marekebisho ya viashiria vya vipimo yamefanywa ili kuwapa wale ambao wamegunduliwa kliniki matibabu ya kiwango cha kawaida kwa kesi zilizothibitishwa ili kuboresha zaidi kiwango cha mafanikio ya matibabu.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kuna kesi 447 kutoka nchi nyingine 24 na vifo viwili nje ya China vilivyoripotiwa Februari 13.
Februari 12, Kamati ya Kudumu ya Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya CPC iliketi kwa mara ya tatu kujadili kuzuia na kudhibiti virusi hivyo.
“Ikiongozwa na Rais Jinping, mkutano huo ulionyesha umuhimu wa kulitatua fumbo la kudhibiti janga kwa kuinua viwango vya kulaza wagonjwa hospitali na viwango vya tiba na kupunguza maambukizi na viwango vya vifo,” ilieleza taarifa hiyo.
WAFANYAKAZI WA AFYA WALIOAMBUKIZWA
Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Afya, Zeng Yixin, amesema wafanyakazi wa afya 1,716 wameambukizwa kuanzia siku ya Jumanne.
Wengine 1,102, wamegundulika kuwa na virusi hivyo.
Idadi hiyo imetangazwa ikiwa ni wiki moja tu tangu raia kuonesha hasira zao kwa mamlaka za taifa hilo kutokana na kifo cha daktari aliyegundua virusi hivyo lakini akazuiliwa na kunyamazishwa na polisi mwezi Desemba.
Serikali ya China inajizatiti kuweka vifaa zaidi vya kujikinga na virusi hivyo katika hospitali zote mjini Wuhan ambako madaktari wamezidiwa nguvu na idadi kubwa ya watu walioambukizwa.