LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM
SERIKALI ya Japan kupitia ubalozi wake nchini, imetiliana saini na halmashauri nne kwa ajili ya kutendeleza miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 819.
Balozi wa Japan nchini, Shinichi Goto, akizungumza wakati wa kusaini mikataba hiyo jijini Dar es Salaam jana, aliitaja miradi hiyo kuwa ni uboreshaji wa mazingira ya elimu katika Tarafa ya Kisesa Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu wenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 203.
Alisema fedha hizo zilizotolewa kupitia mfuko wa maendeleo wa Kisesa zitatumika kujenga madarasa na vyoo na kununua madawati katika Shule ya Sekondari ya Mwakisandu, na kujenga vyoo katika Shule ya Sekondari ya Sakasaka na Shule ya Msingi ya Nzanza.
Mradi wa pili utahususha ununuzi wa magari mawili ya kubebea wagonjwa katika Hospitali ya KCMC ya Moshi mkoani Kilimanjaro msaada ambao unatolewa baada ya hospitali hiyo kutembelewa na Mbunge Mihara Akihiko, kutoka Japan.
“Hivyo Serikali ya Japan imeamua kutoa msaada wa dola za Marekani 52,996, (Sh milioni 118) ambazo zitakwenda kwa Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC) kwa ajili ya kurekebisha na kuingiza ambulance mbili kutoka Japan na manunuzi ya vifaa tiba vitakavyowekwa kwenye ambulance,” alisema Balozi Goto.
Aliutaja mradi mwingine ambao uliotiliwa saini katika hafla hiyo ni wa ujenzi na urekebishaji wa majengo ya zamani katika Shule ya Sekondari ya Kizimkazi katika Wilaya ya Kusini Mkoa wa Kusini Unguja mradi ambao ulipendekezwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Balozi Goto alisema kutokana na ombi hilo, Serikali ya Japan imeamua kutoa msaada wa dola za Marekani 129,596 (Sh milioni 290) kwa ajili ya kujenga madarasa, maktaba, chumba cha walimu na kununua madawati katika Shule ya Sekondari ya Kizimkazi.
“Mradi wa nne ni ujenzi wa maktaba katika Mkoa wa Kilimanjaro ambapo Balozi Dk. Augustine Mhiga alipendekeza mradi huo. Hivyo Serikali ya Japan imeamua kutoa msaada wa dola 90,271 (Sh milioni 202) zitakazokwenda kujenga maktaba hiyo katika kijiji cha Keryo,” alisema Balozi Goto.