TOKYO, Japan
SERIKALI ya Japan imethibitisha kukubaliana na Marekani juu ya umuhimu wa kushirikiana na Urusi na China kumaliza mvutano na Korea Kaskazini inayotuhumiwa kutengeneza makombora ya nyuklia.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Urusi (TASS), makubaliano hayo yalifikiwa juzi katika mkutano wa Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe na Rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye yu ziarani katika nchi za Asia na Pasifiki.
“Tutahakikishia tunaongeza shinikizo ambalo jumuiya ya kimataifa ilihitaji, lakini kupitia ushirikiano wa nchi moja hadi nyingine – Urusi na China, ili kupata suluhisho ya jambo hili.
“Tunaunga mkono msimamo wa Rais Trump, kwamba mikakati yote ipo mezani kwa ajili ya kushughulika na Korea Kaskazini,” alisema Abe katika mkutano wao na waandishi wa habari akiwa na rais huyo wa Marekani.
Waziri Mkuu Abe alisema kwamba ni jambo la muhimu kukaa na Urusi na kuweka mashinikizo kimataifa dhidi ya Korea Kaskazini, ili kuhakikisha inaachana na vitisho dhidi ya mataifa mengine.