Tunu Nassor-Dar es Salaam
Jamii imeshauriwa kuacha matumizi ya vipodozi vyenye viambata vya sumu badala yake watumie vya asili kuepukana na kuharibu ngozi zao na magonjwa ya saratani.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa duka la vipodozi vya asili la Bottega Verde lililopo Mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam, Meneja Masoko wa duka hilo, Cureen Apies amesema matumizi ya vipodozi vyenye viambata vya sumu husababisha uharibifu wa ngozi asili.
“Nitoe ushauri kwa jamii kuhakikisha wanatumia vipodozi vya asili ambavyo hutengenezwa kutokana na matunda na miti asilia,” amesema.
Amesema vipodozi vilivyopo katika duka hilo ni vya asili ambavyo hutengenezwa bila kuongezwa kemikali.
“Asilimia kubwa ya vipodozi vilivyopo hapa dukani ni vyakula na matunda ambavyo huandaliwa mahsusi kwa ajili ya ngozi,” amesema Cureen.
Naye Muuzaji, Merci Mgalla amesema wamejipanga kuhakikisha kuwa wanatoa elimu kwa jamii kuhusu namna bora ya matumizi ya vipodozi.
“Hapa tunatoa elimu bure kwa wanaofika dukani kwetu jinsi ya kupaka vipodozi vyetu na pia namna ya kuchagua vinavyokwenda sambamba na ngozi walizonazo,” amesema Merci.