30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Jamii yakumbushwa kuwajali watu wenye ulemavu

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Jamii imeaswa kuwakumbuka watu wenye ulemavu kwani nao wananafasi muhimu katika kuleta maendeleo ya Taifa.

Wito huo umetolewa leo Jumanne Mei 3, 2022 na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Jamal Katundu, aliposhiriki chakula cha mchana na jamii ya wanafunzi na watumishi wa Chuo cha Ufundi Stadi(VETA) kwa watu wenye ulemavu Yombo cha jijini Dar es Salaam katika kusherekea sikukuu ya Idd el Fitr.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Adam Katundu, (aliyesimama) akizungumza na wanafunzi pamoja na viongozi mbalimbali wa Chuo cha Ufundi cha watu wenye ulemavu Yombo alipotembelea chuo hicho akiambatana na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda (katikati). Wakwanza kulia ni Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Mariam Chelangwa.

“Nitoe wito kwa jamii kwa ujumla kutenga muda wao kwa ajili kujumuika na watu wenye ulemavu ili kuendelea kuwapa faraja na kuwatia moyo wa kuendelea kujituma na kutoa mchango wao katika ujenzi wa Taifa letu kwa kadri inavyowezekana,” amesema Prof. Katundu na kuongeza:

“Kwa upande wetu sisi Serikali tunaendelea kutimiza wajibu wetu wa kuwahudumia Watanzania wote bila kujali hali zao na ndio maana leo tumeona ni vema kujumuika na vijana wetu wenye ulemavu ambao wanapatiwa mafunzo katika chuo hiki ambacho ni miongoni mwa vyuo vyetu vilivyopo katika kanda mbali mbali kwa ajili ya kuwalea na kuwapa ujuzi vijana wenye ulemavu wa aina tofauti ikiwemo uziwi, ulemavu wa ngozi, ulemavu wa viungo nakadhalika.” 

Aidha, Katibu Mkuu huyo amesema serikali imeanza kufanya maboresho ya miundombinu katika vyuo vya ufundi vya watu wenye ulemavu nchini ili kuliwezesha kundi hilo maalum kupata ujuzi muhimu utakaoliwezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli mbali mbali za uzalishaji mali.

“Nadhani mmeshaliona lile gari kubwa ambalo limekuwa likija hapa chuoni, mnajua linaleta nini?” Aliwauliza wanafunzi wa chuo hicho ambao waliitikia “maru maru”.

Kwa mujibu wa Prof. Katundu na Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Mariam Chelangwa, serikali imetenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu mbali mbali yakiwemo mabweni na vyumba vya madarasa katika chuo hicho na vingine vilivyopo Singida, Tabora, Mwanza, Tanga na Mtwara ambapo tayari baadhi ya vifaa vya ujenzi vimeshaanza kufikishwa katika vyuo husika.

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ufundi cha Watu Wenye Ulemavu Yombo, Mariam Chelangwa (wakwanza kulia), akifanya utambulisho wa wanafunzi na viongozi mbalimbali wa chuo hicho wakati Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Adam Katundu, (hayupo pichani) pamoja na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda (katikati) walipotembelea chuo hicho kwa lengo la kujumuika na jamii ya wanafunzi na watumishi wa chuo hicho katika kusherekea sikukuu ya eid el-fitr

Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu huyo ameambatana na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda, ambaye amesema lengo la kuandaa na kushiriki chakula cha pamoja na jamii hiyo ya wanafunzi na watumishi wa chuo ni kuendelea kutoa faraja kwa kundi hilo muhimu katika jamii ambalo mara nyingi limekuwa likisahaulika.

“Tumekuja hapa kwasababu tunatambua kuwa watu wenye ulemavu ni sehemu ya jamii lakini kwa muda mrefu watoto hawa wanakuwa pekee yao pamoja na walezi wao tu hivyo wanatuhitaji sana kwa ajili ya kuendelea kuwatia moyo na kuwafariji. Hivyo, sisi kama Ofisi ya Waziri Mkuu tumeona leo tuje tujumuike nao kwa kula pamoja, kuongea na kucheza nao kama namna ya kuendelea kuwapa faraja na kuwahamasisha kuendelea kujibidiisha katika masomo yao. Na si hivyo tu, kuja kwetu hapa kunatuwezesha kufahamu changamoto zao na kupata mrejesho zaidi wa maendeleo ya vyuo vyetu,” amesema Mwenda.

Kwa upande wao, Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Mariam Chelangwa na mmoja wa wakufunzi wa chuo hicho, Aloyce Nkuna, wamewashukuru viongozi waliowatembelea na serikali kwa ujumla kwa jitahada mbali mbali zinazochukuliwa katika kuwezesha chuo kuendelea kutekeleza wajibu wake kikamilifu.  

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda (wakwanza kulia), akishiriki katika zoezi la kugawa chakula kwa wanafunzi wa Chuo cha Ufundi cha Watu Wenye Ulemavu Yombo alipotembelea chuo hicho akiambatana na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Jamal Adam Katundu (hayupo pichani) kwa lengo la kusherehekea sikukuu ya Idd El Fitr pamoja na wanafunzi na watumishi wa chuo hicho.

Aidha, baadhi ya wanachuo wakiwemo, Joseph Baraza na Asia Bashiri wametoa shukrani zao za dhati kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea kuwakumbuka ambapo viongozi wa Ofisi hiyo wamekuwa wakiwatembelea na kujumuika nao mara kwa mara.

“Tunawashukuru wageni wetu wote mliotutembelea katika siku hii ya leo, tumefurahi, tumekula pamoja nanyi katika sikukuu hii ya Idd El Fitr na tuwaombea kwa Mungu azidi kuwabariki,” amesema Joseph Baraza, Mwanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Yombo.

Wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi kwa Watu Wenye Ulemavu Yombo wakiwasikiliza viongozi mbalimbali wakati wa ziara ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Adam Katundu pamoja na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda katika chuo chicho.

Chuo cha Ufundi Stadi Yombo cha watu wenye ulemavu ambacho kipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kilianzishwa mwaka 1973 kwa malengo ya kutoa mafunzo ya ufundi kwa vijana wenye ulemavu nchini. Chuo kinatoa kozi mbali mbali za ufundi zikiwemo; Ufundi Umeme, Uwashi, Ushonaji, Uchomeleaji Vyuma pamoja na Kilimo na Ufugaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles