32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

JAMII YA WARUHINGYA ILIYOGEUZIWA KISOGO NA DUNIA

NI hulka ya mazoea tege kwa migogoro mikubwa kusababisha dunia kusahau madhila yanayozikumba jamii ndogo.

Maangamizi dhidi yao yamekuwa yakiendelea kwa miongo mingi kama jamii ya Waislamu wa Ruhingya inavyoteseka tangu mwaka 1970 wakilazimika kulikimbia Taifa lao la Burma.

Idadi ya wakimbizi kutoka jamii hiyo wanaojisalimisha mpakani mwa Myanmar na Bangladesh imeongezeka hadi kufikia zaidi ya 250,000 kutoka 150,000 siku chache tu zilizopita.

Jamii hiyo ya Waruhingya imekabiliwa na maangamizi makubwa tangu mwaka 1970 hususani kutoka kwa watu wa jamii inayoamini Buddha.

Yanayofanywa na jamii ya Buddha dhidi ya Waruhingya wanaolazimika kurundikana ugenini kujisalimisha, ni kinyume na wanavyofahamika na wengi duniani kutokana na mfumo wao wa imani kufundisha kujizuia dhidi ya ukatili.

Kuna takribani Waruhingya 200,000 Saudi Arabia, 10,000 katika Falme ya Kiarabu, 350,000 Pakistan, zaidi ya 600,000 Bangladesh, 40,000 India na zaidi ya 150,000 katika nchi za Thailand, Malaysia na Indonesia huku ndani ya Myanmar kwenyewe zaidi ya 100,000 wakiwa wakimbizi wa ndani.

Mgogoro huu unaofukuta katika maeneo yenye Wabuddha wengi katika taifa hilo umesababisha doa kubwa kwa Mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, Aung San Suu Kii, aliyewahi kutumikia kifungo cha muda mrefu cha nyumbani chini ya utawala wa kidikteta wa kijeshi.

Baada ya shinikizo la kimataifa ameingia madarakani kwa chama chake kutawala na kumsababishia mkanganyiko hususani kutoka kwa makundi ya kupigania haki yaliyopaza sana sauti kumtetea wakati akisukwasukwa na manyanyaso ya utawala wa kidikteta.

Kwamba hachukui hatua za kutosha kuzuia mauaji ya jamii hiyo ndogo ambayo haina wa kuitetea na imeamua kuunda makundi yake ya wanamgambo ambayo pia yanapigwa vita na jeshi la Myanmar linalowaua.

Waruhingya wanatangatanga wakikataliwa Bangladesh wanakokataliwa kuwa sio raia licha ya vizazi vyao kuishi kwa miaka mingi, lakini pia nchini Burma wanaonekana kuwa ni wahamiaji wasiotakiwa na ikumbukwe kilichopelekea Suu Kyi kushinda tuzo ya amani miaka 26 iliyopita ni jinsi alivyopigania kutambuliwa kwa jamii ndogo nchini humo.

Lakini kauli yake aliyoitoa siku chache zilizopita akikengeuka na kudai kuwa madhila ya Waruhingya yanatiwa chumvi kuzidisha kuonewa huruma tofauti na hali halisi ilivyo. Waruhingya wanaililia jumuiya ya kimataifa iwaonee huruma kwani wanakabiliwa na mauaji ya Kimbari wasiyostahili kufanyiwa na hakuna anayewajali kwa kuwatetea, wakitangatanga kwa kukosa kutambuliwa uraia wao kwenye nchi zinazopakana.

Licha ya kukosa mahali pa kuishi kutokana na kutotambuliwa wamewekwa mtu kati na wapiganaji wa Kibuddha na jeshi la Myanmar wakiwaua wanawake vikongwe na watoto sanjari na wapiganaji wa Kirohingya, bila kujali kuwa kwa kufanya hivyo wanavunja sheria za kimataifa.

Lakini pia wamesahaulika na serikali ya Su Kyii na jumuiya ya kimataifa inayoonekana kutowachukulia kwa uzito unaostahili. Jimbo la Rakhine ambako wengi wa waliokimbilia ughaibuni wametokea ndiko fukuto la wakimbizi wa sasa wa jamii hiyo lilikoanzia walipokimbilia nchini India, lakini ambako serikali ya nchi hiyo inataka kuwafutia hadhi ya ukimbizi hatua itakayofuatiwa na kufukuzwa kutoka katika taifa hilo.

Kwa kuanza na hatua ya kuwaorodhesha tayari kwa kuwaondoa kwa kudaiwa kuwa kitisho cha usalama, hususani baada ya mashambulizi ya mabomu kwenye hekalu la Kibuddha la Bodhgaya miaka minne iliyopita linaloshutumiwa kutekelezwa na wanamgambo wa Kiruhingya wanaodaiwa kupata mafunzo yao nchini Saudia Arabia ambao wameamua kulipiza kisasi ughaibuni kwa mahujaji wa Kibuddha.

Lakini pia wakihofiwa kutumiwa na maadui wa India wanaotokea Pakistan ingawa India inashutumiwa kwa kuwa ndumilakuwili kwa kuwakataa Waruhingya, kwa kuwa tu imewakumbatia Wabuddha tangu mwaka 1959 walipokimbia maangamizi ya Wachina na kumkaribisha Dalai Lama kiongozi wa Kibuddha duniani anayetoka katika jimbo la Tibet ingawa hadhi yake na wafuasi wake nchini humo hazina ufafanuzi halisi.

Waruhingya ni jamii ndogo yenye Waislamu wengi zaidi miongoni mwao iliyoanza kuishi nchini Myanmar yenye Wabuddha wengi tangu karne nyingi zilizopita, lakini ambao utamaduni wao ikiwemo lugha ya ‘Ruaningga’ wanayoongea ukijitofautisha na jamii nyingine Kusini Mashariki mwa taifa hilo katika eneo la Rakhine.

Hawatambuliki kuwa miongoni mwa jamii rasmi 135 za wazawa wa taifa hilo na kufutiwa uraia wao tangu mwaka 1982 na kusababisha wasiwe na taifa lolote wanalotambulika kuwa kwao.

Jimbo la Rakhine wanalopatikana ni miongoni mwa maeneo masikini kabisa lisilokuwa na huduma muhimu za kijamii lakini pia hawaruhusiwi kutoka nje ya jimbo hilo bila kibali cha serikali.

Licha ya kukataliwa kutambuliwa kwao lakini jamii hiyo ilianza kuishi nchini humo tangu karne ya kumi na mbili wakitokana na watumwa chini ya utawala wa Uingereza wa mwaka 1824 hadi 1948, lakini baada ya Uhuru serikali iliharamisha uraia wa vizazi vya wahamiaji na kusababisha Waruhingya kuchukuliwa kuwa Wabengali waliounda jina la Ruhingya ili kupata hadhi kisiasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles