27.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Jamii na imani potofu ya wagonjwa wa akili

Na AVELINE KITOMARY

 MAGONJWA ya afya ya akili  ni aina ya matatizo ambayo yanaathiri hisia, mawazo na kuleta mabadiliko ya tabia kwa mtu. 

Magonjwa  haya yanaweza kumpata mtu yoyote lakini kuna mambo yanayosababisha au kuleta uhatarishi wa kupata.

Mambo hayo ni kama uwezo  binafsi wa  kupokea na kuchanganua  changamoto mbalimbali mtu anayopitia  na endapo akishindwa  matokeo yake mtu anaweza kuishia kupata tatizo.

 Kitu kingine  kinachoweza kusababisha  magonjwa hayo ni mazingira ambayo mtu anayoishi kama vile kutokupata amani baada ya kukumbana na unyanyasaji.

Jamii inayomzunguka muhusika kutokuwa karibu kumsikiliza inaweza kusababisha  lakini pia tatizo hilo linarithiwa .

Pia kuna magonjwa ya mwili kama malaria kupanda kichwani ,kupata ajali ,kupata tatizo la ubongo, virusi vya VVU  kuharibu ubongo na magonjwa mengine .

Kuna magonjwa yanayoathiri mama mjamzito na mtoto kuzaliwa akiwa   na tatizo mfano sonona kwa mama,pombe,dawa za kulevya ,sigara na mengine.

HALI YA UGONJWA ILIVYO

Kwa mujibu wa shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Watoto Duniani (UNICEF)  kila sekunde 40 mtu mmoja hufarikia dunia kutokana  ugonjwa wa afya ya akili.

WHO pia wameainisha kuwa vijana asilimia 20 ulimwenguni kote wanashida ya afya ya akili na katika nchi za kipato cha kati na chini karibu asilimia 15 wamefikiria kujiua.

Hata hivyo kujiua ni chanzo cha vifo vya vijana wenye umri wa miaka 15-19 duniani kote .

 Hapa nchini takwimu zilizotolewa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) zinaonesha kuwa  kuna ongezeko la wagonjwa wa afya ya akili hadi kufikia asilimia 10.8.

Akitoa takwimu hizo mkuu wa idara ya magonjwa ya afya ya akili, Dk Fileuka  Ngakongwa anasema  wagonjwa waliotibiwa kwa mwaka 2019/2020 Muhimbili -Upanga walikuwa  32,307 ukilinganisha na wagonjwa 21,183 walitobiwa 2018/19.

“Kwa upande wa Muhimbili Mloganzila 2019/2020 wagonjwa waliotibiwa walikuwa ni 980 wakati mwaka 2018/2019 waliotibiwa walikuwa 753 huku ongezeke likiwa ni asimilia  23 Mloganzila.

AINA ZA MAGONJWA YA AKILI

Dk. Ngakongwa  ambaye pia ni Daktari bingwa wa Magonjwa ya akili anasema kuna aina nyingi ya magonjwa ya akili lakini kuna yaliyo maarufu ambayo ni haya.

“Kuna skizofenia wengine wanaita  kichaa japo jina hili huwa hatulipendi linaleta nyanyapaa  huu unachukua asilimia moja ,ugonjwa mwingine ni sonona unatokea sana  kutokana na msongo wa mawazo  huu unaenda hadi asilimia 25 mpaka 35 ni watatu kuleta uzito katika mabadiliko ya afya ya akili.

“Ugonjwa huo pia unaweza  kutokana na kurithi mtu anakuwa na hulka za kuchangamka,uraibu wa dawa za kulevya,hofu ya kupitiliza na mengine ,”anaeleza Dk Ngakongwa.

SABABU YA WANAUME KUWA WENGI

Katika takwimu zilizotolewa na hospitali hiyo idadi ya wanaume imeonekana kuwa kubwa zaidi kuzidi ya wanawake.

Takwimu za mwaka 2018/2019    idadi ya wanaume ilikuwa ni 18,535 huku wanawake wakiwa ni 10,631.

Dk Ngakongwa anasema zipo sababu ya takwimu  hizo kupishana kwa kiwango kikubwa  na hapa anaeleza.

“Afya ya akili inamlenga kila mwanadamu na jinsia zote  lakini ukiangali uwiano kati  ya wanawake na wanaume unatofautiana  mfano nitoe ugonjwa skizofemia(kichaa).

“Hapo uwiano kati ya mwanaume na mwanamke ni mbili ya moja kibaolojia  wanaume wanaweza kupata  mara mbili zaidi ya wanawake na pia wanaume wanawahi haraka kupata kwa umri mdogo  kulinganisha na wanawake lakini ukija kwenye sonona uwiano unaweza kuwa sawa lakini kwa wanaume ni mkubwa zaidi,”anabainisha.

Anasema sababu nyingine ni wanaume kutokuwa wepesi kuongea hata pale wanapokwazwa au kukumbwa na matatizo mbalimbali  hali hiyo huwafanya  kubaki na vitu vingi akilini.

“Wanaume  huwa wanakuwa na siri sana  unaweza kumkera lakini asikuambie  akanyamaza na haongei  wala hata kulia hii ni hatari kwa afya zao vitu vinapomzidi uwezekano  wa kupata tatizo la afya ya akili upo,”anasema.

Oktoba mwaka jana Mwenyekiti wa Chama cha Wataalamu wa Afya ya Akili Tanzania, Isaack Lema aliwasahauri wanaume kulia ili kuweza kukabili msongo wa mawazo ambao unasababisha kujiua.

“Wanume wanaongoza kujinyonga mara tatu kuliko wanawake  hivyo ni bora wakalia au kuongea wanapokubwa na matatizo  ili kupunguza msongo wa mawazo,”anasema Lema.

ASILIMIA 30 YA VIJANA WANA DALILI ZA SONONA

Dk Franck  Mkui ni Daktari bingwa wa magonjwa ya akili na  mratibu wa afya ya akili katika  mkoa wa Dar es Salaam anasema  tafiti zilizofanyika hapa nchini asilimia 30 ya vijana wanadalili za awali za sonona huku asilimia 10 wakihitaji kuonwa na daktari kwa ajili ya tiba.

Anasema licha ya hali ya utoaji huduma kuboreka katika jiji la Dar es Salaam  lakini bado kuna uhitaji wa jamii kuujua ugonjwa wa afya ya akili.

“Nchini Tanzania matibabu za afya ya akili hutolewa katika  hospitali mbalimbali za rufaa,kanda na hospitali ya taifa.

“Hadi sasa katika kliniki zote tatu  za  methadone kuna wagonjwa 6,900 ambao wako kwenye tiba  na ina kadiriwa kuwa kati ya waraibu 10,000 tumeweza kuwafikia  na kuwapa matibabu bure hili ni jambo zuri.

“Waathirika wa dawa za kulevya wanawekwa kwenye kundi kutokana na mabadiliko ya kitabia ambayo yanatokana na ubongo,”anabainisha.

AJIRA, MALEZI  NA VILEVI TATIZO KWA VIJANA  

Dk Mkui anasema ukuaji wa teknolojia na hali za kiuchumi hufanya vijana wengi  kuwa katika hali ya kuathirika afya ya akili.

Anasema hali hiyo inatokea kutokana na wazazi kutokumuandalia  mazingira mazuri tangu akiwa  mtoto.

“Malezi wanayopata hayawajengei uwezo wa kujitegemea baadae  hivyo wanapokua na kujitegemea hawajui ni jinsi gani wanaweza kukabiliana na changamoto za maisha  hasa za kazi.

 “Wengine  walikuwa wanapewa kila kitu hawajui  kufua nguo,hajui kusafisha nyumba  sasa anapoenda kwenye mazingira mapya anapata ‘stress’ (msongo wa mawazo) na  inapozidi anapata sonona  kutokana na kutokuzoea maisha.

“Kingine ni ugumu wa maisha  hakuna urahisi wa ajira kama ilivyokuwa mwanzo huchangia kijana kuwa na mawazo mengi na kupata sonona,”anaeleza Dk Mkui.

Anasena sababu zingine ni matumizi ya dawa za kulevya ,pombe,sigara na vilevi vingine.

“Ni muhimu kuwapa vijana elimu hasa pale wanakuwa shule ili waweze kuelewa madhara ya hivyo vitu na pia tunawasaidia kuweza kukabili hali ya afya ya akili ikiwemo ukosefu wa ajira.

“Lakini kingine kuna wazazi hawana tabia ya kukaa na watoto wao muda mwingi wako ‘busy’ na kazi

Sasa utakuta mtoto hata akiwa na tatizo hapati mtu wa kumsikiliza au wa kumfatilia maendeleo yake hii inaweza kuwa sababu moja wapo  ya tatizo la afya ya akili,”anasema,

WAGONJWA KUCHELEWA,UNYANYAPAA CHANGAMOTO

Msaikolojia tiba wa magonjwa ya afya ya akili kutoka hospitali ya Muhimbili, Isaack Lema  anasema changamoto zilizopo ni wagonjwa wengi kuchelewa kufika hospitali .

“Changmoto nyingi  ni unyanyapaa au kujinyanyapaa mwenyewe kwa mgonjwa ,kuna watu wanawanyanyapaa wagonjwa hali hii hufanya wajisikie vibaya.

“Lakini pia kuna wagonjwa wengi kulinganisha na uwezo ila  tunajitahidi kuwahudumia wote matibabu ni bure lakini kuna dawa zingine wanachangia hivyo mwenye bima anapewa na wakati mwingine ukosefu wa fedha ni changamoto pia,”anafafanua.

Lema alitoa wito kwa jamii kuendelea kuimarisha afya zao za akili pindi wanapokutana na matatizo mbalimbali ambayo hupelekea msongo wa mawazo.

“ Suala la afya ya akili ni muhimu kwa kila mtu hivyo hata waliougua wanavyopona huweza kufanya kazi zao mfano waathirika wa dawa za kulevya na wagonjwa wa akili wakipewa mafunzo baada ya kupona wanaweza kuzalisha .

“Hivyo ni muhimu wagonjwa  kufika au kuwafikishwa vituo vya afya mapema watu wenye viashiria vya magonjwa ya akili ili waweze kupata tiba kwa kuwa magonjwa ya akili yanatibika.

UELEWA WA JAMII

Lema  anasema bado jamii haina uelewa  wa kutosha kwani  wengine wahahusisha na ushirikina na mtu  anaponesha dalili hawawezi kumsaidia.

“Bado jamii inahitaji elimu zaidi wajue kuna magonjwa ya akili yanayoweza kutokea katika jamii

Ili wajue jinsi ya kumsaidia mtu kabla hajafikia hatua ya kujiua.

“Ni tatizo kubwa wagonjwa wengi kabla ya kufika hospitali wanakuwa wamezunguka sana wengine wanaenda kuombewa au kwa waganga wa kienyeji

Wakiona hawaponi  wanaletwa hospitali kwa makaridirio ni asilimia 50,”anabainisha.

Anashauri jamii kufuatilia taarifa za afya ya akili ili anapotokea mgonjwa aweze kuwahishwa hospitali haraka.

“Mgonjwa anapowahishwa hospitali uwezekano wa kupona haraka ni mkubwa  kuliko vile akichelewa nawashauri jamii kuacha  kuwaza zaidi imani za kishirikina kwa kuwa huo ni ugonjwa kama yalivyo magonjwa mengine hivyo wagonjwa wawahishe hospitali,”anashauri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles