Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA
WAZIRI wa Nchi, ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, amewataka watumishi wa wizara hiyo kujipima na kujitafakari katika utendaji wao wa kazi.
Alisema wale wanaodhani hawawezi kufanya kazi kwa kasi ya sasa bora wakae pembeni.
Jafo alitoa kauli hiyo mjini hapa jana alipokuwa akijitambulisha kwa watumishi wa Tamisemi baada ya kuapishwa wiki iliyopita.
Alisema kutokana na hali ya sasa na ukubwa wa wizara, kila mtendaji anastahili kufanya kazi kwa kiwango kikubwa ambacho kitakuwa na manufaa kwa serikali na jamii kwa ujumla.
Alisema kamwe hataweza kuwavumilia watumishi ambao wanafanya kazi kwa mazoea na bila kutimiza wajibu wao.
Waziri aliwataka kujipima na kujitafakazi katika utendaji wao wa kazi.
Vilevile aliwataka watumishi wote kuwa na mipango kazi ambayo inatekelezeka na kutoa ripoti ya kazi zao iliyo sahihi na siyo ripoti ya kupikwa.
Jafo aliwaagiza wakurugenzi wa kila idara kuhakikisha wanawapatia mipango kazi watumishi na kuwapima kwa viwango vyao vya kufanya kazi.
Alisema ikionekana kuna mtumishi ambaye hawezi kufanya kazi kwa viwango vinavyotakiwa ni bora akakaa pembeni.
“Napenda kusema kuwa kwa sasa sitaki kuona mtumishi anafanya kazi kwa mazoea.
“Katibu mkuu nakuagiza tupangiane kazi na kazi hiyo ipimwe kwa viwango vinavyotakiwa ili kazi iweze kuleta tija kwa serikali na kwa jamii.
“Hapa TAMISEMI siyo dampo la kuleta watumishi wa kujirundika ofisini, badala yake kila mtumishi atoke ofisini na afanye kazi yenye tija, afanye kazi yenye tija kwa serikali na kwa jamii kwa ajili ya maendeleo.
“Tuna shule 22 za serikali ambazo ni vipaji maalumu, jambo la ajabu hazipo hata ndani ya 10 bora.
“Lazima tujiulize ni kwa nini zinakuwa nyuma katika elimu, tufanye kila juhudi kuhakikisha shule hizo zinafanya vizuri,”alisema.