Na Mwandishi Wetu, Kilwa
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Kilwa kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo.
Waziri huyo ambaye yupo katika ziara ya kikazi mkoani Lindi, ameanza kutembelea Wilaya ya Kilwa ambapo alikagua miradi miwili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Somanga na madarasa katika Shule ya Msingi Singino.
Pia amekagua Kituo cha Afya Somanga ambapo alipita kila jengo kisha kutoa tathmini yake ya kuridhishwa na ujenzi huo.
“Mheshimiwa mkuu wa mkoa nimeridhwa na ujenzi huu, naomba nitumie nafasi hii bila kificho kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hii ndugu Renatus Mchau kwa usimamizi mzuri wenye matokeo makubwa.
“Nimezunguka katika halmashauri zote nchini najua hali halisi, naomba niwapongeze kwa umoja wenu na kuwahakikishia kuwa hiki kituo cha afya kitakuwa bora nchini,” amesema Jafo.
Kituo hicho kilianza kujengwa mwaka 2017 baada ya wananchi wa kata hiyo kumsimamisha Rais Dk. John Magufuli na kuomba kujengewa ambapo rais alitoa Sh milioni 20 na baadaye halmashauri ilianza kwa mapato yake ya ndani na baadaye waliwatafuta wadau wa maendeleo kampuni ya uchimbaji gesi nchini (Pan Africa Energy) ambao walikubali kushirikiana na kisha kukamilisha ujenzi huo kwa zaidi ya Sh milioni 700.
Mpaka sasa kituo hicho kimekamilika kwa asilimia 98 na Mkandarasi Kampuni ya Wanyumbani Constraction Company Ltd yupo katika hatua za mwisho kukabidhi mradi huo.
Kituo hicho kina majengo saba muhimu ambayo ni jengo la wagonjwa nje (OPD), jengo la upasuaji, maabara, wodi ya akina mama, jengo la kufulia, jengo la kuhifadhia maiti pamoja na sehemu ya kuchomea taka.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Gofrey Zambi, amemuhakikishia Waziri Jafo usimamizi mzuri wa miradi yote katika mkoa huo ambapo kwa mara ya mwisho ulipokea zaidi ya Sh bilioni tano kwa ajili ya miradi mbalimbali katika wilaya zote.
Kwa upande wake Mkugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Renatus Mchau, amemshukuru Waziri Jaffo na kumhakikishia kuwa yeye na timu yake wataendelea kusimamia miradi yote na itakamilika kwa wakati.
“Kwa sasa tuna ujenzi wa madarasa katika shule mbalimbali na katika Kata hii ya Somanga tumekarabati madarasa matatu Shule ya Msingi Somanga na tumeanza ujenzi wa madarasa mengine mawili, ukarabati wa madarasa hayo pia ulichagizwa na mchango wa Rais Magufuli baada ya kutoa mchango wa shilingi milioni tano na kisha halmashauri ilitoa shilingi milioni thelathini ili kukamilisha madarasa matatu,” amesema Mchau.
Pia amesema katika Shule ya Msingi Singino ujenzi unaoendelea ni wa madarasa mawili na matundu saba ya vyoo kwa Sh milioni 47 zilizotolewa na Serikali katika mpango wa maboresho ya shule za msingi na sekondari nchini.
Katika Kipindi cha miaka mitatu Halmashuri ya Wilaya ya Kilwa ilipokea fedha kwa ajili ya maboresho ya vituo vya afya vitatu ambavyo ni Tingi, Pande na Nanjirinji ambavyo ukarabati wake umekamilika kwa asilimia 100 na vimeanza kutoa huduma kwa wananchi.
Kituo cha Afya somanga kinatarajiwa kuanza kutoa huduma mara tu vifaa vitakapofika kwa kuwa ujenzi wa miundombinu umekamilika .