Na JANETH MUSHI,ARUSHA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Suleiman Jafo, amekemea mpango wa kubadilishwa matumizi ya Sh milioni 400 zilizotolewa kwa ajili ya upanuzi na ukarabati wa Kituo cha Afya cha Kaloleni.
Fedha hizo zilitumwa kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya kituo hicho na alidai kushangazwa kutaka kutumika kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Moshono.
Akizungumza jijini hapa jana alipotembelea kituo hicho kilichopo katika Halmashauri ya Jiji la Arusha alisema kinatoa huduma kwa wananchi wengi huku miundombinu yake ikiwa hairidhishi na kuahidi kutafuta fedha kwa ajili ya kukikarabati na kukipanua ikiwa ni pamoja na kujengwa kwa chumba cha kuhifadhia maiti, chumba cha upasuaji na chumba cha joto cha watoto njiti.
“Msinitibue asubuhi hii, nilikuja hapa nikakuta wataalamu wanafanya kazi katika mazingira mabaya, kuna shida sana hapa, nikaahidi kutafuta fedha tukatuma shilingi Milioni 400 tangu Juni 26, mwaka huu lakini nashangaa hamjatekeleza,” alisema na kuongeza:
“Hapa mnataka muhamishe goli, fedha mnataka kuzipeleka kituo kipya cha afya cha Moshono, nawaagiza muanze ujenzi Jumatano ijayo na kituo hiki na hadi Novemba 30, mwaka huu ukarabati uwe umekamilika.”
Awali Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Dk. Simon Chacha, alikiri fedha hizo kutolewa kwa kuwa walipanga kuzitumia kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Moshono na cha Kaloleni walipanga kukikarabati kwa kutumia fedha za mapato ya ndani.
Hata hivyo, Jafo, alipingana na maelezo hayo na kumtaka kuhakikisha wanaanza ujenzi wa kituo hicho na kuhusu kituo cha afya cha Moshono alimtaka hizo fedha walizotaka kutumia kutoka katika vyanzo vyao vya mapato wazitumie kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.