DAMASCUS, SYRIA
NDEGE za jeshi la Israel zimeripotiwa kushambulia kwa makombora uwanja wa ndege wa jeshi la Syria jana, huku Marekani na Ufaransa zikikanusha kuhusika na mashambulizi hayo.
Awali Rais wa Marekani, Donald Trump na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, waliapa kuchukua hatua kali dhidi ya utawala wa Syria baada ya majeshi ya nchi hiyo kudaiwa kufanya shambulizi la silaha za sumu dhidi ya raia mjini Douma.
Shambulizi hilo la sumu limelaaniwa vikali na jumuiya ya kimataifa na jana Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitarajiwa kufanya kikao cha dharura kulijadili.
Serikali ya Syria na mshirika wake Urusi, ambazo awali zilielekeza kidole Marekani, zimeishutumu kwa shambulio la jana lililoua askari 14.
Shambulio hilo liliulenga uwanja wa ndege za kivita wa Tiyas unaofahamika kwa umaarufu kama T4, karibu na mji wa Homs.
Israel ambayo awali iliwahi kuyalenga maeneo ya Syria, bado haijatoa tamko lolote.
Tukio hilo limetekelezwa huku jamii ya kimataifa ikiendelea kulaani shambulio la kemikali ambalo lilitekelezwa katika mji wa Douma unaoshikiliwa na waasi, huku Marekani na Ufaransa zilitishia kulipiza kisasi.
Rais wa Marekani, Donald Trump alimweleza Rais wa Syria kama ‘nduli’ na kuonya yeye pamoja na washirika wake Iran na Urusi ‘watalipia uovu wao’.