TEHRAN, IRAN
UONGOZI wa ran umepuuza wito kutoka Marekani na Umoja wa Ulaya (EU) wa kuitaka iache mpango wake wa kutengeneza makombora.
Hata hivyo Jamhuri hii ya Kiislamu imesema haina mipango ya kuongeza uwezo wake wa kutengeneza makombora ya masafa marefu.
Waziri wa Ulinzi wa Iran, Amir Hatami amenukuliwa na Shirika la Habari la Tasnim akisema maadui wanataka nguvu za Iran za kutengeneza silaha zivunjwe.
Alikumbushia msimamo wao kuwa suala la uwezo wao wa kutengeneza makombora si suala la kujadiliwa.
Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa wa Iran, Ali Shamkhani, pia amesema nchi yake itaendelea kuufanyia kazi mpango wake wa kuunda makombora.
Shamkhani ambaye ni mshirika wa karibu wa kiongozi wa dini mwenye ushawishi mkubwa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, amesema nchi hiyo haina vikwazo vya sayansi wala ufundi kuongeza nguvu zake za jeshi.
Rais wa Marekani, Donald Trump aliiondoa nchi yake kutoka kwa makubaliano ya mataifa kuhusu mpango wa nyukilia wa Iran na kuirejeshea nchi hiyo vikwazo vya uchumi.
Marekani ilitumia hoja kuwa makubaliano hayo kati ya nchi zenye nguvu zaidi duniani na Iran hayakuangalia suala la uwezo wa Iran kutengeneza makombora na ushawishi wake katika masuala ya kanda ya Mashariki ya Kati.