BAGHDAD, IRAK
IRAK inawania kurejesha jukumu lake la uongozi katika mataifa ya Kiarabu baada ya miongo kadhaa ya mzozo, ambapo viongozi wake wana nia ya kuendeleza uhusiano mzuri na Iran na Marekani.
Kumekuwa na wimbi la shughuli za kidiplomasia pamoja na ziara za ngazi ya juu mjini Baghdad, ikiwa ni pamoja na kufunguliwa tena kwa ubalozi mdogo wa Saudi Arabia, kwa mara ya kwanza kipindi cha karibu miaka 30.
Irak inajitokeza kutoka katika vita viharibifu vya miaka mitatu dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu na inakabiliwa na mzigo mkubwa wa ujenzi mpya na kuwarejesha mamia kwa maelfu ya watu waliokimbia makazi yao.
Rais Barham Salih ameliambia Shirika la Habari la Associated Press katika mahojiano mwezi uliopita kwamba wakati umewadia kusema ‘tunahitaji utaratibu mpya wa kisiasa, ambao utashuhudia Irak ikirejea kuwa nguzo muhimu katika kanda hii.