28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

IMF YAUNGA MKONO JITIHADA ZA JPM

Na SAID AMEIR – MAELEZO

SHIRIKA la Fedha Duniani (IMF) linaziunga mkono jitihada za Rais Dk. John Magufuli za kupambana na vitendo vya rushwa na ukwepaji wa kodi, kwa kuwa hiyo ni sehemu ya kielelezo cha dhamira ya kweli ya Serikali yake ya kuleta maendeleo kwa faida ya wananchi wote.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IMF, Dk. Tao Zhang, alisema Dar es Salaam jana kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika kukuza uchumi wake na kupata mafanikio katika sekta ya huduma za jamii, ambayo ni matokeo ya kazi nzuri na sera madhubuti za uchumi.

 “Uchumi wenu umekua kwa kiwango cha wastani wa asilimia 7 katika miaka ya hivi karibuni na viashiria vya maendeleo katika sekta ya jamii ni vizuri.

 “Kwa mfano kupungua kwa vifo vya watoto wachanga kwa asilimia 60 na uandikishaji wa watoto elimu ya msingi umeongezeka kwa asilimia 36,” alisema.

 Dk. Zhang alisema hayo wakati akitoa mada kuhusu “kufikia mafanikio: Tanzania kufikia lengo la kuwa nchi ya kipato cha kati” katika  Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Alisema kutokana na mwenendo wa sasa wa ukuaji wa uchumi, Tanzania iko katika nafasi nzuri ya kupata mafanikio zaidi, ikiwamo kuwa nchi ya kipato cha kati kama ilivyoelezwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2020.

 “Kuna mambo mengi ambayo yanatoa fursa kwenu, ikiwamo uanachama wenu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, rasilimali ambazo zimo mbioni kupatikana katika miaka ya karibuni na rasilimali watu kubwa na iliyoelimika,” alisema Dk. Zhang.

Aliwaambia washiriki wa mhadhara huo kuwa kitu muhimu sasa kwa Tanzania ni kuendelea na usimamizi mzuri wa uchumi na kusimama katika kuchukua hatua kufungua fursa zake za maendeleo.

Alisema kama zilivyoweza kufanya nchi nyingine, anaamini Tanzania inaweza kufikia hatua hiyo.

Dk. Zhang aliainisha maeneo matatu muhimu ambayo Tanzania ikiyafanyia kazi ipasavyo yataleta mabadiliko makubwa na kuipaisha nchi katika ngazi nyingine ya juu ya maendeleo.

Aliyataja maeneo hayo kuwa ni kuongeza uwekezaji kwa kushughulikia vikwazo vinavyozorotesha uwekezaji na kuongeza nafasi za ajira.

Nyingine ni kuchukua hatua madhubuti kuimarisha nafasi ya sekta binafsi katika uchumi na kuongeza kasi ya ukuaji uchumi na kuhakikisha mafanikio yanayopatikana yanamfaidisha kila mwananchi kwa kupata fursa za elimu, afya na huduma za fedha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles