Aveline Kitomary -Dar es salaam
DAKTARI Bingwa wa Macho, kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Dk. Ombi Jao amesema kuwa imani potofu imekuwa ikiwachelewesha watoto wengi kupata matibabu ya saratani ya macho mapema.
Dk. Jao alisema hayo jana jijini Dar es Salaam katika mahojiano na Gazeti la Mtanzania, ambapo alitoa ufafanuzi wa kina kuhusu ugonjwa wa saratani ya macho kwa watoto.
Kwa mujibu wa daktari huyp alisema kuwa takribani watoto 100 hadi 150 huonwa kila mwaka wakiwa na tatizo hilo na kupata huduma kwenye vituo vya tiba hapa nchini.
“Wengi wa watoto hawa hufika katika Hospitali ya Muhimbili, KCMC, Bugando na Hospitali ya Rufaa ya Mbeya. Takribani asilimia 70 hadi 90 ya watoto hawa hufikishwa Muhimbili wakiwa kwenye hatua ya juu ya ugonjwa hali hiyo husababisha asIlimia 50 hadi 70 ya watoto kupoteza maisha kwasababu ya kuchelewa kupata tiba inayostahili na utafiti wetu unaonesha kuwa imani potofu imekuwa kikwazo kikubwa,” alisema Dk. Jao.
Alisema ni vyema wazazi kuwawahisha watoto hospitali kwani matibabu ya saratani ya macho yapo endapo mtoto atawahishwa atapona kabisa.
“Changamoto tunayoipata sisi ni watoto kuja wamechelewa licha ya imani potofu pia watoto hawa wanapita kwenye vituo mbalimbali za afya wanapewa dawa za matone na matibabu ya muda mrefu huko, tunachotakiwa kujua ni kwamba sio kila dawa ya matone ni dawa inayotibu jicho nawashauri kuwa mpeleke kituo cha afya ukiona anaendelea msogeze kituo kingine.
“Tunatoa matibabu kutegemeana na hatua ya saratani aliyopo mtoto mfano hatua za mwanzo kuna matibabu ambayo hayauhusishi kutoa jicho ni ya kuua uvimbe kwa kuchoma mionzi kama ni mdogo unaweza kuweka dawa za kansa ndani ya macho au kuna namna ya kugandisha na barafu jicho mara kadhaa na baada ya muda uvimbe unakufa kabisa.
“Lakini pia kuna matibabu ya kwenye mishipa ya damu tunapitisha dawa tunaita ‘thermotherapy’ inazunguka inaua chembechembe hizo, ikishindikana kabisa ikiwa iko katika hatua ya juu ni salama kutoa jicho kabisa ili kumsaidia maisha ya mgonjwa kwasababu saratani inaweza kusambaa hadi kwenye ubongo akapaoteza maisha,” alisema Dk. Jao
Alisema matibabu mengine ni ushauri nasaha kwani wakati mwingine mzazi anapata shida sana mtoto anapopoteza jicho.
“Kwasababu inaumiza na wakati wa kushauria unakuwa mgumu mpaka wengine wanatoroka wanaenda kwa waganga wa kienyeji au ukishindwa kumsaidia kuelewa siku akirudi saratani imeshasambaa na huwezi kuokoa tena maisha yake kwahiyo tunakuwa na wakati mgumu wa mashauriano,” alibainisha.
Alisema dalili za saratani hiyo ni jicho kutoa mwanga wenye rangi nyeupe ambao huwaka kama jicho la paka usiku.
“Dalili nyingine ni kengeza, jicho linakuwa halioni hivyo ubongo unadharau hilo jicho unakazana ni linalofanya kazi, jicho kuwa jekundu,jicho linatoa machozi na wakati mwingine ikifikia hatua mbaya linavimba kabisa na kutoka nje,”alieleza.
Dk. Jao alisema saratani ya jicho huweza kurithiwa kutoka kwa kizazi kimoja hadi kingine hivyo ndugu waepuke kuoana ili kupunguza hatari ya kupata magonjwa ya kurithi.
“Kwa wale wanaooana kutoka kwa familia moja wanaweza kuambukizana kwasababu vinasaba vina uhusiano kwahiyo watoto wanaweza kurithi.
Alishauri wazazi kujijengea utamaduni wa kuwapima watoto macho mara kwa mara ili kugundua kama kunatatizo mapema.