Na NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM
MATOKEO ya utafiti mpya wa kitaifa kuhusu upatikanaji na utumiaji huduma za kifedha nchini (Finscope), yanaonyesha kuwa asilimia 28 ya Watanzania bado hawajafikiwa na huduma za kifedha, huku ule wa mwaka 2013 ukionesha ambao walikuwa hawajafikiwa na huduma hiyo walikuwa ni asilimia 26.
Hata hivyo, utafiti wa mwaka huu ambao ni wanne kufanyika nchini umehusisha watu milioni 27.8 wakati ule wa 2013 ulihusisha watu milioni 24.
Akizungumza jana wakati wa kutangaza matokeo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Kukuza Sekta ya Fedha nchini (FSDT), Sostenes Kewe, alisema. “Huduma za kifedha zinahusisha mikopo, kuweka akiba au amana, huduma za malipo na miamala mingine. Huduma hizi ni za muhimu kwa watu kujiendeleza na kujikwamua kiuchumi,” alisema.
Akizungumzia viwango vya elimu vya watu waliohojiwa kwenye utafiti wa mwaka huu, alisema asilimia 3 wana elimu ya juu, asilimia 18 (sekondari), asilimia 64 (msingi) na asilimia 15 hawajaenda shule kabisa.
Alisema utafiti huo uliangazia uelewa wa watu kuhusu masuala ya fedha, watu walio nje ya mfumo wa sekta ya fedha na mambo wanayopaswa kuzingatia watoa huduma ili waweze kuwafikia wananchi kwa ukaribu.
Alisema taarifa ya matokeo ya utafiti huo itasambazwa kwa watunga sera na kwa watoa huduma za kifedha ili waweze kuboresha huduma na kuwafikia wananchi kwa karibu.
GAVANA
Akizungumza baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Beno Ndulu, alikiri kuwa licha ya kukua kwa teknolojia, bado watu wengi hawatumii huduma za kifedha.
Alitolea mfano wa mitandao ya simu aliyosema imewafikia asilimia 95 ya Watanzania wote na wanaoweza kutumia simu za mkononi ni asilimia 86.
“Kwa kutumia mitandao ya simu ni njia rahisi na haina bugudha, gharama yake ni nafuu kuliko njia tulizokuwa tunatumia kabla, lakini kuna watu hawaitumii kabisa katika huduma za kifedha.
“Inawezekana hawajui huduma hizi na namna ya kuzitumia ama ni suala la kutokuwa na kipato… Itabidi tuliangalie kwa karibu,” alisema Profesa Ndulu.
Alisema hata kwa wale ambao wamefikiwa na huduma hizo, bado kuna changamoto juu ya namna gani ya kuzitumia.
Kuhusu mchango wa mabenki kuwa mdogo katika kusukuma mbele sekta hiyo, alisema bado hajaona kama ni tatizo.
Kulingana na utafiti huo kati ya benki 56 ni benki sita tu ndizo zilizoshika soko la fedha nchini.
“Ni kweli benki sita kubwa zinatoa huduma karibu asilimia 60 lakini mimi bado sijaona hatari kwa sababu kunakuwa na unafuu wa gharama kulinganisha na benki ambayo ni ndogo,” alisema.
WIZARA YA FEDHA
Mchumi Mkuu kutoka Wizara ya Fedha, Dionisia Mjema, alisema sheria ya mfumo wa malipo iliyotungwa mwaka juzi, imesaidia kampuni za simu na benki kushirikiana katika utoaji huduma na kuwafikia watu wengi.
“Benki zikiweza kuwafikia wananchi na kutoa mikopo mikubwa hasa katika kukuza agenda ya Tanzania ya Viwanda matokeo yajayo yanaweza kuwa mazuri zaidi,” alisema Mjema.
ZANZIBAR
Katibu Mtendaji Tume ya Mipango Zanzibar, Juma Reli, alisema kwa Zanzibar watu ambao hawapati huduma za kifedha ni asilimia 42 na hali hiyo imechangiwa na utamaduni wa baadhi ya watu wa Pwani.
“Watu wengi katika maeneo ya Pwani na baadhi ya mikoa hawaamini kuweka fedha zao benki, wanaamini kuweka kwenye godoro au mfukoni, hii kiuchumi sio nzuri kwa sababu haiwasaidi kupata huduma za kifedha,” alisema Reli.
Alisema asilimia 70 ya fedha ndani ya uchumi ziko nje na watu mmoja mmoja ndio wanasababisha hali hiyo kwa kuwa nje ya mfumo rasmi wa kifedfha.
“Kiasi cha fedha ambacho kiko ndani ya mikono ya watu kinakuwa kingi sana, tuweke mikakati ya kuhakikisha tunaondokana na utarattibu wa watu kuweka fedha zao nyumbani na kuweka katika mifumo rasmi,” alisema.