Na WAANDISHI WETU, DAR/MIKOANI -
VIONGOZI wa dini katika makanisa mbalimbali nchini, wametoa ujumbe mzito katika ibada ya Sikukuu ya Krismasi, huku wakitaka uwepo wa utawala wa kidemokrasia nchini.
Pia wamekemea vitendo vya ukatili, ikiwamo matukio ya utekaji nyara na mauaji ya kinyama, hali inayotishia kutoweka kwa amani ya nchi iliyoasisiwa na waasisi wa taifa kwa miaka mingi.
Viongozi hao wa kiroho, wakiwamo maaskofu na wachungaji, walitoa mahubiri hayo wakati wa ibada zilizofanyika jana asubuhi na kwenye mkesha wa Krismasi.
Akihubiri jana katika ibada ya Krismasi ambayo kitaifa ilifanyika Zanzibar, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar, Augustine Shao, alisema siasa safi ndiyo msingi wa Tanzania, hivyo kuna haja ya tofauti za mitazamo ya kisiasa kuheshimika na kila mtu.
Askofu Shao alisema mfumo wa vyama vingi umesaidia katika kukosoa, kutofautisha na kutoa uwazi serikalini, hivyo ni vyema kuheshimu mawazo.
Alisema ishara mbaya ni katika uchaguzi mdogo uliofanyika Novemba 11, mwaka huu kwa wahusika kushindwa kufahamu namna ya misingi bora ya demokrasia inavyotakiwa kuwa.
“Katika chaguzi ndogo zilizopita kulikuwa na mizengwe ya hapa na pale iliyoendelea, haikufaa kwani imekiuka demokrasia. Tunatakiwa kutambua kuwa siasa ni kama mchezo wa mpira, mnamaliza kushinda kisha mnakuwa marafiki,’’ alisema Askofu Shao.
UCHUMI
Katika hatua nyingine, askofu huyo alisema licha ya kukua kwa uchumi, lakini umasikini mkubwa umeongezeka miongoni mwa Watanzania.
Alisema wakati uchumi umekua, umaskini kwa Watanzania umeongezeka huku baadhi ya viongozi wakiwa matajiri kupitiliza.
Askofu Shao aisema hali ya viongozi wa kisiasa kiutajiri inatisha jambo ambalo linashangaza kwani wakiingia madarakani wanatangaza idadi ya mali zao, lakini baada ya kuongoza kwa muda wanakaa kimya.
Alisema kukaa huko kimya ni dalili kwamba wamekuwa wakiomba nafasi mbalimbali za uongozi ili kutaka kujifungulia milango ya utajiri na kujilimbikizia mali.
“Viongozi wengi wanataja mali zao kabla ya kuingia madarakani na baada ya hapo hutowasikia tena wakitaja, kwanini wanafanya hivyo?” alihoji Askofu Shao.
Pia aliwataka viongozi kufanya mambo kwa haki ya kweli kwa kujali wananchi na kujifunza kujinyima ili watu wote wawe na haki sawa, huku akieleza hakuna mabaya au maovu yatakayoshinda mema.
“Mungu ameagiza tuwe wahanga kuondoa giza kwa wenzetu ili haki na amani iweze kupatikana kwa kila mtu,’’ alisema.
Askofu huyo alisisitiza kila aliyeshiba anatakiwa kumjali mwenye njaa na kwamba kila mtu afanye aliyoagizwa na Mungu kufanya.
AJIRA KWA VIJANA
Askofu Shao ameitaka Serikali kuwasaidia vijana waliokosa mikopo na wasio na ajira wapate ajira kwani vijana ni muhimu katika taifa lolote.
Alisema vijana wengi waliomaliza vyuo licha ya kusoma kwa bidii na kufanikiwa, wamekuwa wakihangaika mitaani bila mafanikio, hivyo ameitaka Serikali isaidie katika eneo hilo.
“Vijana wetu wanahitaji ajira ili nao waweze kufurahia maisha, ni vizuri Serikali iwasaidie katika kusoma na kupata ajira kwani yapo mataifa kwa sasa yanateseka kwa kushindwa kuendeleza vijana wao,’’ alisema.
Alisema kama vijana hawatasaidiwa, Tanzania ya viwanda inayotarajiwa itakuwa ni ndoto kufikiwa.
Askofu Shao pia aliwataka wafanyabiashara wakubwa kulipa kodi kwa wakati ili iweze kusaidia nchi katika harakati za maendeleo.
Alisema wanafunzi kukosa ada na dawa hospitalini kunasababishwa na wafanyabiashara wakubwa kukwepa majukumu yao ya kulipa kodi na kulinyonya taifa.
“Serikali ya awamu ya tano inasisitiza uwajibikaji, ukusanyaji wa kodi ni haki na wajibu kwa kila mfanyabiashara kuzingatia hilo ili maendeleo ya nchi yaweze kupatikana.
“Wakwepaji wengi wa kodi ni wafanyabiashara wakubwa na hao hao ndio wamekuwa waharibifu wakubwa wa miundombinu yetu.
“Mfano wanaofanya biashara kwa kutumia magari makubwa wanaharibu barabara, lakini ndio hao hao ambao leo wamekuwa wakwepa kodi,’’ alisema Askofu Shao.
WAFUNGWA HURU
Pia alimpongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kuwaachia huru wafungwa, huku akiamini waliopo magerezani wakiwamo vijana, wataendelea kujirekebisha na kuwa na tabia njema inayompendeza Mungu na jamii nzima.
Askofu Shao alisisitiza amani nchini kwa kujitakasa upya hasa katika Sikukuu ya Krismasi, huku akiwataka Watanzania kila mmoja kuheshimu mawazo ya mwenzake hata kama wanatofautiana.
PENGO NA HOFU YA MUNGU
Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amewataka Watanzania kutenda matendo mema huku wakiongozwa na hofu ya Mungu.
Akizungumza jana wakati wa misa ya pili ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, Askofu Pengo alisema maendeleo hayawezi kuja kama Watanzania wenyewe hawana maadili au hofu ya Mungu.
Askofu Pengo alisema kila mmoja awe mwananchi au kiongozi, anapaswa kuwa na hofu ya Mungu ambayo itamwongoza katika kufanikisha mipango iliyokusudiwa.
Alisema pia Watanzania wanapaswa kukubali kuongozwa na kuwaombea viongozi wao ili kuhakikisha jitihada zinazofanywa zinazaa matunda.
“Naunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Magufuli na Serikali katika kuleta maendeleo, lakini hatuwezi kufanikiwa kama hakuna maadili.
“Hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha kuwa anakuwa na maadili na hofu ya Mungu, jambo ambalo linaweza kutusaidia kufikia malengo yaliyokusudiwa,” alisema Askofu Pengo.
Alisema katika maisha ya kila siku binadamu wanapaswa kumtegemea Mungu kwenye shughuli mbalimbali ili kufanikisha mipango wanayokusudia.
“Hatuwezi kupata maendeleo kwa njia ya mkato halafu hatuna maadili wala hofu ya Mungu, kwa sababu naamini mwisho wa siku tutaishia kubaya, hivyo basi kila mmoja anapaswa kuwa na hofu hiyo ambayo itamwongoza katika mipango yake,” alisema.
Alitoa mfano wa nchi mbalimbali ambazo zilikuwa zinahangaikia maendeleo kwa kumtegemea Mungu na mwisho walifanikiwa na kupata maendeleo hadi sasa.
Alisema Watanzania wanapaswa kujifunza kutoka kwenye nchi hizo ili waweze kufanikiwa malengo yao.
Askofu Pengo alisema nchi ambazo zilipiga hatua bila ya kumtegemea Mungu wala kutokuwa na maadili mwisho ziliishia kubaya na kufilisika kabisa.
Alisema Watanzania wanapaswa kujirekebisha makosa yao na kuongozwa kwa maadili na kufanya kazi kwa bidii ambayo itawasaidia kufanikisha malengo yao na kupata maendeleo.
“Wananchi wakiwa na maadili, nchi inafanikiwa na kupiga hatua za maendeleo, hivyo basi kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha kuwa anasimamia maadili na hofu ya Mungu ili nchi iweze kufanikiwa,” alisema.
Alisema anatambua kuwa binadamu anapotafuta maendeleo anatumia njia nyingi ili kuhakikisha anafanikiwa, lakini kikubwa ni kuhakikisha kuwa unapoangaikia suala hilo, lazima uwe na hofu ya Mungu ambayo itakuongoza ili kufikia malengo yako.
HOFU KWA WANANCHI
Kwa upande wake, Askofu wa Jimbo Katoliki Moshi, Isack Amani, amekemea vitendo vya ukatili kama vile utekaji nyara na mauaji ya kinyama yanayoendelea nchini kuwa vinatishia kutoweka kwa amani iliyopiganiwa na waasisi wa taifa kwa miaka mingi.
Akihubiri katika ibada ya Krismasi iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Kristu Mfalme Moshi, Askofu Amani, alisema katika kipindi cha muda mfupi nchi imekumbwa na matukio mbalimbali jambo linalohatarisha kutoweka kwa amani.
Alisema kutokana na kuendelea kwa matukio hayo, hofu imetawala miongoni mwa wananchi jambo ambalo ni tofauti na miaka ya nyuma
“Uvamizi wa vituo vya polisi, ulevi wa kupindukia, ulegevu wa imani za dini, mauaji ya kinyama yakiwamo ya wazee, ni baadhi tu ya mambo yanayotokea nchini na kuzua hofu kwa wananchi. Dalili hizi ni mbaya na zinaashiria kutoweka kwa amani yetu,” alisema.
Alisema ni vema mamlaka husika zikachukua hatua mapema ili kudhibiti hali hiyo ambayo imeonekana kuwakosesha amani Watanzania.
“Mamlaka husika ni vema wakachukua hatua stahiki haraka ili kudhibiti matukio haya ya kinyama yanayoendelea kwani Tanzania tuliyonayo sasa si ile ya miaka ya nyuma,” alisema.
SHOO AONYA VITISHO
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Fredrick Shoo, amesema kumekuwepo na watu wanaotishwa na kujengewa hofu ili kushindwa kutoa maoni yao kulingana na kile wanachokiamini katika taifa lao.
Dk. Shoo alisema watu wanapaswa kusimama katika kweli na kuacha woga wa kuyasema yale wanayoyaona ni sahihi katika kulijenga taifa.
Aliyasema hayo wakati akihubiri katika ibada ya Krismasi iliyofanyika jana KKKT Usharika wa Moshi Mjini mkoani Kilimanjaro.
Askofu Shoo ambaye pia ni Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini, alisema katika kusimamia kweli watu wasiyumbishwe na kujikuta wanaogopa kusema na kutoa maoni ya kile wanacho kiamini.
“Tusione woga wa kutetea kile tunachokiamini, kuna baadhi ya watu wanajaribu kuwajaza wengine hofu na kuwatisha ili wasiseme ukweli na kutoa mawazo yao kwa kile wanachokiona,” alisema Askofu Shoo.
Alisema Watanzania wanapaswa kuwa wakweli katika Kristo licha ya kwamba katika ukweli huo kuna watu watakaowachukia.
Mbali na hilo Askofu Dk. Shoo, aliwataka Watanzania kutobaguana kwa itikadi za kisiasa, kiuchumi, kikanda na kikabila.
Alisema ni wakati wa kushirikiana na kuhakikisha wanadumisha mshikamano na amani ya nchi ambayo ilipiganiwa kwa muda mrefu na waasisi wa taifa.
MALASUSA AHIMIZA UPATANISHO
Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa, amewataka Watanzania kutumia Sikukuu ya Krismasi kupatana na kuwa wamoja.
Akizungumza katika ibada ya Krismasi iliyofanyika katika Kanisa la Azania Front, Dar es Salaam, Askofu Malasusa alisema kuna watu wengi wanaishi bila kupatana hata ndani ya kanisa.
“Neema inatuagiza kukataa dhambi na inatukumbusha kuwa watu wa kutafuta amani na upatanisho.
“Lazima tuwe patanishi, tuukatae ubaya, ugomvi, tupatane. Watu wasiishi kwa kuangalia macho chini kwa sababu wako wengine hata ndani ya kanisa wanaishi bila kupatana,” alisema.
Pia aliwatahadharisha waumini wa kanisa hilo kuacha kuhangaika kwenye madhehebu na badala yake watambue kuwa anayeweza kuwabadilisha ni Mungu na wala si binadamu.
“Nyakati tunazoishi si za kawaida, wapo wengi wanahangaika na makanisa na siku hizi watumishi tumebadilisha majina mengi tu, lakini tutambue kuwa Yesu ndiye atakayekubadilisha na si mwanadamu,” alisema.
Askofu huyo pia alitawataka Watanzania kujiepusha na matendo maovu na kuwa mawakala wa amani.
“Tuukatae ubaya wa aina yoyote, wizi wa mali za umma, uvivu, uzembe na mengine mengi. Watu wanatakiwa wayaone matendo yako na si mpaka wasikie jina zuri,” alisema.
Pia aliwatia moyo wale wote waliokata tamaa na kusema kuwa suluhisho pekee ni kumfuata Yesu Kristo.
“Kuna watu wamekataliwa na wenyewe wanajikataa, hata wale ambao dhambi zao zimedhihirishwa Yesu anawahitaji.
“Zimepita Krismasi nyingi, lakini hii iwe ya kipekee, Yesu Kristo azaliwe mioyoni mwetu,” alisema Askofu Malasusa.
RUVUMA
Askofu wa KKKT Dayosisi ya Ruvuma, Amon Mwenda, amewataka waumini wa kanisa hilo kujiimarisha katika nyanja mbalimbali zikiwamo za kiuchumi ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya kidunia.
Akitoa salamu za Sikukuu ya Krismasi wakati wa ibada, alisema waumini wanatakiwa kutambua kuwa dunia ya sasa imebadilika, hivyo ni vyema wakajifunza kubadilika katika nyanja mbalimbali zikiwamo za kiuchumi.
Alisema kama waumini watakubali kuingia kwenye mabadiliko hayo, yatawafanya waendane na ulimwengu wa sayansi na teknolojia, ambao unahitaji kutumia elimu ili kufanikiwa zaidi.
Alifafanua kuwa changamoto za kiuchumi zimekuwa zikiathiri hadi makanisa na si jamii pekee, hivyo bila uchumi injili itakwenda kwa muda ambao haukustahili.
IRINGA
Kwa upande wake, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Iringa, Blaston Gavile, amewataka Watanzania kuacha kulalamika kuhusu vyuma kukaza na badala yake kumrejea Mungu awapiganie wafanikiwe kimaisha.
Akizungumza mara baada ya ibada katika Usharika wa Kanisa Kuu, Askofu Gavile alisema Wakristo hawana sababu ya kuungana na wanaolalamika vyuma kukaza bali wanapaswa kufanya kazi na kumtanguliza Mungu kwa kila jambo.
“Tunalalamika vyuma vimekaza kwa sababu hatufanyi kazi kwa juhudi na maarifa, Rais Dk. Magufuli kila wakati yupo kwa ajili ya kututumikia na kuona Taifa linasonga mbele,” alisema Askofu Gavile.
Alisema jukumu kubwa la viongozi wa dini na Watanzania ni kuendelea kuiombea nchi amani na kumwombea Rais Magufuli ili aendelee kuwatumikia Watanzania vema.
“Kazi anayoifanya rais wetu ni nzuri na sisi tunazidi kumwombea aendelee kuifanya na zaidi azidi kuzingatia katiba yetu kama anavyofanya,” alisema.
MTOKAMBALI ATAHADHARISHA
Viongozi wa dini nchini wametakiwa kuzingatia wajibu wao katika kutoa huduma za kiroho na kuacha kuingiza siasa katika nyumba za ibada.
Hayo yalisemwa na Askofu Mkuu wa Makanisa ya Tanzania Assemblies of God (TAG), Dk. Barnabasi Mtokambali, katika imaadhimisho ya miaka 43 ya kanisa hilo yaliyofanyika mkoani Morogoro.
“Viongozi wa dini wanaaminiwa na kundi kubwa la watu, lakini baadhi yao wamekuwa wakitumia nyumba za ibada kama majukwaa ya siasa,” alisema Dk. Mtokambali.
Alisema kitendo hicho kinabadili mitazamo ya waumini na kuacha kuzingatia mafundisho ya kiroho.
Askofu huyo aliwataka viongozi wa dini kuishi kutokana na mafundisho wanayoyatoa kwa jamii ili kuwa kielelezo na mfano wa kuigwa.
Naye Mchungaji Kiongozi Kanisa la TAG Sabasaba Morogoro, Anania Aloyce, alisema baadhi ya viongozi wa dini hawaishi kile wanachokifundisha na kuwataka wabadilike kimatendo.
Kwa upande wake Mbunge wa Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood (CCM), ambaye pia alihudhuria ibada hiyo, alisema Serikali haina dini na kuwaomba viongozi wa dini wanapokuwa na jambo la kuishirikisha Serikali wasisite kufanya hivyo.
DODOMA
Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT), Dk. Dickson Chilongani, amesema viongozi wa Serikali na dini wanatakiwa kujishusha kwa wananchi wa hali ya chini ili kusikiliza kero zao badala ya kujikweza na kuwasahau.
Akizungumza wakati wa ibada ya Krismasi iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu Mjini hapa, Askofu Dk. Chilongani alisema tabia ya viongozi kujikweza imekuwa ikiwakatisha tamaa watu wa chini ambao kwa sehemu kubwa wanawategemea viongozi wao.
“Wabunge na madiwani wanapoomba kura huwa wanyenyekevu, lakini wakishapata hujiweka juu mahali ambako wapigakura wao hawawezi kufika, tabia hii ikiachwa itajenga matabaka,” alisema Askofu Chilongani.
Aliwataka viongozi wengine kuiga mfano wa Rais Dk. John Magufuli ambaye amekuwa akijishusha na kuwatetea wanyonge.
Alisema analofanya Rais Magufuli lilifanywa na Yesu Kristo mwenyewe aliyeshuka na kuwa mwanadamu ili aweze kuwa na watu wote.
Naye Askofu wa Kanisa la International Evangelism Sinai la Ipagala mkoani hapa, Silyvester Tadey, aliwaonya waumini juu ya matumizi ya anasa katika kipindi cha sikukuu.
Akihubiri kwenye ibada ya Krismasi, Askofu Tadey aliwataka watunze akiba kwa ajili ya watoto wao watakapokwenda mashuleni.
Kwa upande wake, Mchungaji Evance Chande wa Kanisa la Evangelism Assembless of God Tanzania (EAGT) Soloam la mjini hapa, amewataka Watanzania kuisheherekea sikukuu hiyo kwa kuisaidia Serikali katika kuhakikisha ulinzi unakuwepo badala ya kuliachia Jeshi la Polisi pekee.
MBEYA
Mchungaji wa KKKT Usharika wa Mbeya Mjini, Amani Mwaijande, amesema ili nchi iweze kukua kiuchumi na kufikia malengo iliyojiwekea, ni lazima wananchi wakubali kuumia kwa kipindi kifupi.
Akizungumza na MTANZANIA baada ya ibada ya Sikukuu ya Krismasi iliyofanyika katika Usharika wa Mbeya Mjini, mchungaji huyo alisema nchi zote zilizoendelea duniani wananchi wake waliumia wakati wa utekelezaji wa mipango endelevu ya kukuza uchumi, hivyo amewataka wananchi kutokuwa wepesi wa kukata tamaa.
Baadhi ya waumini waliohudhuria ibada hiyo walisema viongozi wote waliopita na waliopo wamekuwa na utaratibu wa kuiendesha nchi, hivyo hakuna sababu ya wananchi kulalamika, zaidi ni kujipanga kimkakati.
“Ukiangalia kila kiongozi alikuwa na utaratibu wake wa kuendesha nchi, kwahiyo hatuna sababu ya kulia maisha magumu, tujikite katika kufanya kazi,” alisema mkazi wa Mbeya, Adamu Mbaliezi.
Nao Elizabeth Joseph, Aminaery Richard na Esther Mwakiboke, walimwomba Rais Magufuli kuwaangalia wajasiriamali wadogo kwani wengi wanashindwa kuendesha biashara zao kutokana na kudaiwa na taasisi za kibenki.
Kwa upande wake, Mchungaji wa Kanisa la Moravian Jimbo la Kusini Magharibi, Braison Mwampashi, amewataka Wakristo kusherehekea Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya kwa kumwogopa Mungu badala yake wakumbuke matendo ya Yesu yaliyo mema.
Akizungumza katika ibada ya Sikukuu ya Krismasi iliyofanyika katika Ushirika wa Ruanda jijini Mbeya, Mchungaji Mwampashi alisema wanadamu wanatakiwa watende matendo mema ya kumpendeza Mungu na si kumuudhi.
“Unaposema wewe ni Mkristo, hakikisha kweli unatenda yale yanayompendeza Mungu,” alisema Mchungaji Mwampashi.
TANGA
Mchungaji wa KKKT Ushirika wa Mikanjuni, Warehema Chamshama, amewataka Wakristo kuacha kutenda maovu ili waweze kuwa wapya kwa Kristo kuzaliwa mioyoni mwao.
Sambamba na hilo, aliwaasa kuacha kutoa na kupokea rushwa kwani jambo hilo ni baya na linasababisha haki na wajibu kupindishwa.
“Wakati huu mwokozi Yesu anazaliwa lazima tukae kwenye maadili yanayompendeza Mwenyezi Mungu kwani kazi tulizonazo ni mipango yake, tuhakikishe tunaishi kwa upendo na amani na jamii zinazotuzunguka,” alisema Mchungaji Chamshama.
Habari hii imeandaliwa na Nora Damian, Asha Bani, Patricia Kimelemeta (Dar), Eliud Ngondo, Upendo Fundisha (Mbeya), Ashura Kazinja (Morogoro), Upendo Mosha (Kilimanjaro), Amon Mtega (Ruvuma), Francis Godwin (Iringa), Ramadhan Hassan (Dodoma) na Oscar Asenga (Tanga).