Membe alizaliwa Novemba 9, 1953 katika Kijiji cha Rondo-Chiponda, Wilaya ya Lindi.
Ni mtoto wa pili kati ya saba wa familia ya Mzee Kamillius Anton Ntanchile na Mama Cecilia John Membe.
Alianza elimu ya msingi mwaka 1962 katika Shule ya Rondo – Chiponda na alihitimu mwaka 1968, baadaye akajiunga na masomo ya sekondari katika Seminari ya Namupa mwaka 1969 na kuhitimu kidato cha nne mwaka 1972, kisha akajiunga na kidato cha tano na sita katika Seminari ya Itaga mkoani Tabora mwaka 1973 na kuhitimu mwaka 1974.
Inaelezwa kuwa kabla ya kujiunga na Seminari ya Itaga aliwahi kusomea upadre kwa miezi kadhaa, akiwa miongoni mwa vijana 11 walioshawishiwa na alichaguliwa kujiunga na Seminari Kuu ya Peramiho, Songea.
Ndoto ya Membe kusomea upadri huko Peramiho ilianza kufifia baada ya kufaulu vizuri kidato cha nne, jambo ambalo lilimfanya Askofu Mkuu wa Jimbo la Mtwara wakati huo, marehemu Maurus Libaba, amshawishi ajiunge na Itaga Seminari kusoma kidato cha tano na sita.
Membe alijiunga na JKT, kwa mujibu wa sheria na kufanya kazi serikalini kwa muda wa miaka miwili kama sehemu ya kutekeleza Azimio la Musoma lililowataka watu wote waliomaliza kidato cha sita kufanya hivyo kabla ya kujiunga na chuo kikuu.
Baada ya kumaliza JKT, aliajiriwa katika Ofisi ya Rais na kufanya kazi kwa miaka sita kabla ya kujiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alikopata Shahada ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma kuanzia mwaka 1980 hadi mwaka 1984.
Japokuwa ufaulu wake ulikuwa wa daraja la kwanza, alikataa kuwa mhadhiri msaidizi kwa sababu mwajiri wake alimtaka arejee kazini baada ya kuhitimu masomo.
Akiwa mtumishi katika Ofisi ya Rais alihudumu kama mchambuzi wa masuala ya Usalama wa Taifa kazi ambayo anaelezwa kuifanya kwa mafanikio.
Mwaka 1990 alijiunga na Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, Marekani na kupata Shahada ya Uzamili ya Uhusiano wa Kimataifa na kuhitimu mwaka 1992.
Baada ya kuhitimu pamoja alihamishiwa Wizara ya Mambo ya Nje mahali alipokaa kwa miaka tisa kuanzia mwaka 1992 hadi 2000) akihudumu kama mshauri wa mabalozi, kabla ya kujiunga katika siasa za moja kwa moja.
SAFARI YA KISIASA
Safari yake kisiasa ilianza mwaka 2000 wakati wa Uchaguzi Mkuu alipoomba ridhaa ya ubunge Jimbo la Mtama mkoani Lindi kwa tiketi ya CCM ambapo aliibuka mshindi wakati huo akiwa na umri wa miaka 47.
Mwaka 2005, alitetea kiti hicho baada ya kuwashinda wagombea wenzake, Isack Wolfgans (TLP) na Said Mtepa (CUF).
Januari mwaka 2006 Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani nafasi ambayo alidumu nayo kwa miezi tisa hadi Oktoba alipomhamishia Wizara ya Nishati na Madini kama Naibu Waziri na kuhudumu kwa mwaka mmoja hadi Novemba 2007.
Desemba 2007, aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akichukua nafasi ya Dk Asha-Rose Migiro nafasi ambayo aliitumikia hadi mwaka 2015 utawala wa Rais Kikwete ulipofikia tamati.
Ikumbukwe kuwa wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM mwaka 2015 Membe alikuwa miongoni mwa watia nia wa chama hicho na alifanikiwa kuingia tano bora na baadaye kushindwa kutinga katika tatu bora baada ya kuangushwa na Rais Dk. John Magufuli, Balozi Asha Rose Migiro na Balozi Amina Abdallah.
Mwisho