Na Lilian Justice, Morogoro
KILA binadamu anatamani kuishi hadi kufikia umri wa uzee. Lakini si kila mmoja wao hupata fursa hii.
Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya wazee duniani imeongezeka zaidi katika nchi zinazoendelea, ambapo viwango vya ongezeko hilo havilingani na uwezo wa rasimali hivyo kushindwa kumudu kuwahudumia.
Inatarajiwa kuwa ifikapo mwaka 2050 idadi ya wazee itaongezeka na kuzidi ile ya watoto na vijana chini ya miaka 24. Idadi hiyo katika Bara la Afrika inategemewa kuongezeka kutoka milioni
38 ya sasa na kufikia milioni 212 ifiapo mwaka 2050.
Aidha, ongezeko hilo la wazee linachangiwa na juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na serikali katika kuboresha huduma ya afya.
Katika Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani, iliyofanyika Oktoba mosi, mwaka huu mkoani Dodoma, Shirika la Kuhudumia Wazee Morogoro (MOREPEO) liliwakutanisha wazee wa kata zote 29 za Manispaa ya Morogoro.
Mkurugenzi wa shirika hilo, Samson Msemembo anasema wazee mkoani Morogoro wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo utambuzi na usajili wa wazee, ukosefu wa mabaraza maalumu ya wazee, kukosa fedha za kujikimu na hivyo kuishi maisha magumu.
Msemembo anasema kutokana na changamoto hizo wazee wengi wamekosa kutambulika na kupatiwa huduma ikiwamo zile za afya.
Msemembo anasema wazee hao huachiwa mzigo wa kulea yatima walioachwa na wazazi wao kutokana na kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.
“Wazee ndio huwa na jukumu la kulea yatima na hata walio na maambukizi ya VVU na hivyo kuwafanya wataabike,” anasema Msemembo.
Anasema katika manispaa hiyo, ni mabaraza machache tu yaliyoundwa katika ngazi ya kata ambazo ni Kihonda, Bigwa, Mwembesongo, Tungi na Kikalakala.
Anashauri Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kuandaa mipango na mikakati ya kukamilisha matarajio ya kuunda mabaraza hayo.
Kwa upande wake Mwasilishaji wa mada ya uundwaji wa mabaraza ya wazee, Hussein Msengi anasema katika nchi nzima halmashauri ambazo tayari zimekuwa mstari wa mbele kuunda mabaraza hayo ni pamoja na Magu, Mbarali, Kilosa na Korogwe, jambo ambalo linawarahisishia wazee kukutana na kujadili changamoto zao.
Anasema wazee wamekuwa wakiuawa kinyama kwa kukatwa mapanga, kwa kuhusishwa na imani za kishirikina.
Anasema mauaji hayo yameshamiri zaidi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kama Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Mara, Geita na Kagera ambapo takwimu za mwaka 2015 zinaonesha zaidi ya wazee 700 waliuawa kikatili, sawa na wastani wa wazee wawili huuawa nchini kila siku.
“Kwa hapa Morogoro hatuna takwimu zozote zilizojitokeza za mauaji ya wazee, hivyo tunapaswa kuungana kupinga mauaji yanayotokea katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa kuwa yanalitia doa Taifa,” anasema.
Anataja changamoto nyingine kuwa ni ukosefu wa upatikanaji wa wataalamu wa magonjwa ya wazee kama maradhi ya kibofu cha mkojo.
“Wazee wamekuwa wakikosa dawa pindi wanapoenda kutibiwa na kulazimika kununua maduka ya nje, jambo ambalo wengi wao wanashindwa kumudu gharama na hata kusababisha kuhatarisha maisha yao.
“Ili kuhakikisha changamoto hii inapatiwa ufumbuzi wa kudumu ni lazima kuwapo kwa kliniki malumu ya wazee,’’ anasema.
Kwa upande wake Ofisa Ustawi wa Jamii na Mratibu wa wazee Manispaa ya Morogoro, Joanitha Mashasi anasema utambuzi wa wazee umeanza kufanyika tangu mwaka jana baada ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk. Steven Kebwe kuagiza kila wilaya kuanza kuwatambua wazee wote walioko katika maeneo hayo.
Mashasi anasema wamefanikiwa kuwatambua wazee 2,566 kwa kipindi cha mwaka jana kupitia watendaji wa mitaa na kata.
“Pia tunaendelea na zoezi la kuwatambua wazee wote ambao bado hawajatambuliwa,” anasema Mashasi.
Naye Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro, Baraka Jonas anasema wanahakikisha wazee wote wanatibiwa bure na tayari halmashauri imetenga bajeti hiyo.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Pascal Kihanga anaeleza kuwa ndani ya miezi miwili halmashauri itakuwa imeshasimimia zoezi la kuwatambua wazee wote na kuunda mabaraza ya wazee katika kata zote 29 za manispaa ya Morogoro.
Mzee Elibariki Kweka na Peter Rashid wanasema bado serikali haijaweka mfumo mzuri wa kuwapa huduma bora wazee hususani wakulima hawajaweza kuthaminiwa kama wale waliopo serikalini katika suala zima la kupata huduma bora ya afya ama kulipwa pensheni.
“Wazee wanapaswa kupatiwa huduma bora za afya bila kujali kama alikuwa ameajiriwa serikalini au mkulima. Serikali inapaswa kuhakikisha sera ya wazee inatekelezeka kwa vitendo ili waweze kunufaika kama ilivyo katika nchi zilizoendelea ambazo zinawalipa wazee pensheni hadi mwisho wa maisha yao,” anasema Kweka.