24.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Hospitali Maswa yaanza kutoa huduma kwa watoto njiti

Na Samwel Mwanga, Maswa

HOSPITALI ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imeanza kutoa matibabu kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati “Watoto Njiti” baada ya kupokea vifaa kutoka Taasisi ya Dorris Mollel Foundation.

Mganga Mfawidhi wa hospitali ya wilaya hiyo, Dk. James Bwire, ameyasema hayo mara baada ya kutembelewa na Waandishi wa Habari za afya waliotaka kufahamu juu ya matibabu ya watoto njiti mara baada ya kupokea vifaa vya matibabu kwa watoto hao miezi minne iliyopita.

Amesema kuwa mara baada ya kupata vifaa hivyo vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 50 waliviweka kwenye wodi maalum ambayo inawahudumia watoto hao ili waishi kama wengine.

Amesema kuwa changamoto ilikuwa kubwa kwa sababu wengi wa watoto hao walikuwa wanapoteza maisha kutokana na ukosefu wa vifaa tiba katika hospitali hiyo.

“Moja ya changamoto tuliyokuwa tunaipata kutokana na vifo vya watoto katika hospitali ya wilaya yetu ni hawa watoto njiti na hii ilitokana na kutokuwa na vifaa tiba kwa ajili yao, hivyo wengi wao tulikuwa tunawapatia rufaa kwenda hospitali ya Bugando jijini Mwanza.

“Kuzaliwa njiti si mkosi kama baadhi ya watu wanavyodhani kwenye jamii sasa matibabu yanapatikana hapa na tangu tumeanza huduma hii tumekuwa tukipata watoto wa namna hii kutoka hospitali nyingine za wilaya katika mkoa wa Simiyu maana hospitali yetu ndiyo pekee yenye kutoa matibabu hayo,”amesema Dk. Bwile.

Amesema  watoto wanaozaliwa kabla ya wakati unaweza kuwahudumia kwa njia ya asili ya Kangaroo au ngozi kwa ngozi lakini kuna wale wanaozaliwa na uzito mdogo zaidi chini ya gramu 500 wanahitaji vifaa maalum ili waweze kuishi wakiwa hospitalini.

Naye Mganga Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk. Adorat Mpollo amesema kwa hali ya sasa mama aliyepata mtoto njiti analazimika kubeba gharama za matunzo ya huyu mtoto hasa pale panapohitajika huduma maalum kama za dawa za kukomaza mapafu na dawa hizo ni gharama na dozi moja inauzwa kati ya Sh 500,000 hadi 600,000.

“Mtoto anaweza kuhitaji hadi dozi tatu ili aweze kuwa sawa, kununua mipira ya kulishia iwapo mtoto hawezi kunyonya maziwa ya mama yake hii ni gharama kubwa sana lakini kwa sasa hapa wanapata matibabu bure mara baada ya kupata vifaa hivi,”amesema Dk. Mpollo.

Naye Maria John ambaye amejifungua mtoto njiti na anaendelea kupata matibabu katika hospitali hiyo amesema kuwa watoto wa namna hiyo huhitaji hadi maziwa ambayo ni ghali mno.

Aidha, ameiomba serikali kuelimisha jamii kuanzia wanafunzi hadi kushirikiana na wizara inayohusika na masuala ya afya ili kuanzisha mtaala wa kusaidia elimu ya watoto njiti kwenye mtaala wa Tanzania ili tupate wananchi wenye uelewa wa jinsi ya kujikinga ama kujisaidia ili wasipate mtoto njiti.

“Na hii itasaidia na hata akija mtu kupata mtoto njiti asione kuwa si riziki au mtoto huyu hatoishi na watoto njiti wanaishi tukiwapatia maisha bora,” amesema.

Takwimu zinaonesha kuwa kila mwaka duniani watoto milioni 15 wanazaliwa njiti, yaani ujauzito ukiwa haujatimiza wiki 37 wakiwa na uzito mdogo na uwezo mdogo wa kumudu maisha yao.  

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles